Sibuka FM

Magembe wa Sunzula atupwa jela miaka 30

5 September 2025, 2:44 pm

Muonekano wa nje wa jengo la mahakama ya wilaya ya Itilima ambapo imefanyika hukumu ya kijana Yosia Magembe mkazi wa kijiji cha Sunzula Picha na Anitha Balingilaki

Hatuwezi kuendelea kuona wanafunzi wa kike wanashindwa kufikia malengo yao kisa tu kunamwanaume mmoja mwenye tamaaa zake na wanafunzi lazima sheria ifuate mkondo wake serikali yetu imeweka mazingira ya elimu ili kila mtanzania apate elimu”.

Na,Anitha Balingilaki

Mahakama ya wilaya ya Itilima iliyopo mkoani Simiyu  imemhukumu ,Yosia Paulo Magembe umri miaka 20 mkazi wa kijiji cha Sunzula kilichopo wilayani humo kwenda jela miaka30 kwa kukutwa na hatia ya makosa matatu.

Hukumu ya shauri la jinai Na.19541/2025 imesomwa mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa wilaya ya Itilima Roberth Kaanwa  ambapo kosa  la kwanza ni  kutorosha binti chini ya umri wa miaka 16 Kinyume na kifungu cha 134 cha sheria ya kanuni ya   adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2023  ,kosa la pili ni kubaka  kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha  sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2023 na kosa la tatu kumpa mimba mwanafunzi Kinyume na kifungu cha 62(3) cha sheria ya elimu sura ya 353 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2023 .

Awali Mahakamani hapo , imedaiwa na mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka wilaya ya Itilima inspector  Jaston Mhule  kuwa tarehe 08/08/2025 katika Kijiji cha Sunzula kilichopo  wilayani  Itilima mshitakiwa alimtorosha  mhanga ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili jina limehifadhiwa bila ridhaa ya  wazazi wake, alimbaka na kumsababishia ujauzito.

Taarifa zilifika kituo cha polisi  na  mshtakiwa alikamatwa  akiwa na mhanga na  alifikishwa kituo cha polisi kwa mahojiano baada ya upelelezi kukamilika ilibainika mshtakiwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi huyo tangu July 2025 ndipo  mshtakiwa alifikishwa mahakamani tarehe 12/08/2025.

Jumla ya mashahidi 05 na vielelezo 04 vilitolewa na upande wa mashtaka na baada ya ushahidi huo mshtakiwa alijitetea mwenyewe  na ndipo Mahakama ya wilaya ya Itilima ilimtia hatiani mshitakiwa .

Baada ya kutiwa hatiani upande wa mashtaka uliomba mshitakiwa apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa jamii kwani tukio hilo linamadhara makubwa kwa mhanga kwa kupata ujauzito akiwa mtoto na pia linamkatisha ndoto za kimasomo mwanafunzi na ikizingatia serikali imetenga bajeti kubwa kwaajili ya kutoa elimu bure. 

Mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza  na ndipo hakimu mkazi mwandamizi wa wilaya ya Itilima,Roberth Kaanwa alimhukumu adhabu ya  kwenda jela kifungo cha miezi 09 kwa kosa la kwanza kutorosha binti chini ya umri wa miaka 16,miaka 30 jela kwa kosa la pili la kubaka na mwaka 01 jela kwa kosa la tatu kumpa mimba mwanafunzi na  adhabu  zote zinaenda kwa pamoja hivyo atatumikia miaka 30 jela.