Sibuka FM
Sibuka FM
2 September 2025, 5:21 pm

Nendeni mkasimamie shughuli za maendeleo kwenye vijiji vyenu, muone uchungu wa fedha za miradi zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, mzuie wizi wa fedha na vifaa kwenye Miradi ya maendeleo ” DC Maswa Dkt Vicent Anney ”
Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu wamepewa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao na usimamizi wa Miradi ya maendeleo .
Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe, Dkt Vicent Naano Anney amewataka wenyeviti hao kwenda kusimamia miradi ya maendeleo ili kukuza uchumi wa Wilaya na mtu mmoja mmoja
Mhe, Dkt Anney amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani maendeleo na mipango yote inatoka kwa wananchi ambao wenyeviti wa Vijiji na vitongoji ndio wasimamizi katika maeneo hayo hivyo ni watu muhimu kwa Dira ya maendeleo ya Vijiji

Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya katika Ufunguzi wa Mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ndugu Maisha Mtipa amesema kuwa wameshirikiana na chuo cha Serikali za mita Hombolo Dodoma kutoa elimu kwa Wenyeviti hao ili waweze kujua majukumu pamoja na taratibu za uendeshaji wa shughuli za Serikali
Ismail Juma Kalunde ni Mhadhiri katika Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma (Hombolo) amesema kuwa wenyeviti hao ndio wasimamizi wakuu katika miradi ya maendeleo hivyo wanawapa uelewa wa sheria zinazounda Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na manunuzi katika mamlaka hizo.
Baadhi ya wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo kwani yataenda kuwakumbusha majukumu yao na mambo wanayotakiwa kufanya kwa wananchi ikiwemo usimamizi wa miradi ya maendeleo


