Sibuka FM
Sibuka FM
10 June 2025, 10:24 am

“Hakuna sheria inayobagua watoto kutokana na mapungufu ya kimaumbile, binadamu wote kwa Mungu wetu sote tupo na haki hivyo ni wakati sasa kwa jamii kuachana na imani kuwachukulia watoto wenye mahitaji maalum kama vile ni mkosi, tuwapatie mahitaji yao kama watoto wasiokuwa na ulemavu wowote wa kimwili”.
Na, Daniel Manyanga
Wazazi na Walezi wenye watoto walio na mahitaji maalum wilayani Bariadi mkoani Simiyu wametakiwa kutowaficha ndani badala yake wawapeleke shuleni kwa ajili ya kupata haki yao msingi kwa mjibu wa sheria na haki za watoto bila kujali mapungufu waliyonayo.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Elimu Maalum wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Nasuna Henry wakati akizungumza na maafisa elimu, maafisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuwabaini na kuwatambua watoto wenye mahitaji maalum kwa ufadhili wa mradi wa shule bora huku mratibu wa mradi huo katika halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Felister Mwanga, amesema kuwa mafunzo hayo kwa washiriki yatawasaidia kutambua watoto wenye mahitaji maalum kwa weledi zaidi kwa kushirikiana na walimu.
Kwa upande wao Enock Pwele na Rutherford Magayane ambao ni wawezashaji wa mafunzo hayo wameeleza namna ambavyo yatawasaidia washiriki wa mafunzo hayo kufanya kazi ya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum kwa weledi.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo, Maro Msami ambaye ni afisa elimu kata ya Ngulyati na Wamdenge Kalingonji ambaye ni afisa ustawi wa jamii wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi wamesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi tofauti na hapo mwanzo kabla ya kupata ujuzi huo.