Sibuka FM
Sibuka FM
5 June 2025, 8:59 pm

“Hakuna maendeleo ya vitu kama watu wako hawana miundombinu rafiki ya barabara maana ndiyo njia Kuu ya wananchi kupiga hatua kimaendeleo maana wakipata shida ya kiafya watawahi kwenye matibabu lakini hata biashara itakuwa katika maeneo husika”.
Na, Daniel Manyanga
Askofu wa Jimbo katoliki la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu,ameiomba serikali mkoani Simiyu kuboresha miundombinu ya barabara ya Bariadi – Nkololo ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa huduma za afya wanapokwenda kutibiwa katika kituo cha afya cha Songambele kinachomilikiwa na kanisa katoliki hali itakayowafanya wagonjwa kuwahi Kupata matibabu.
Askofu Sangu ametoa ombi hilo wakati akizungumza katika misa ya jubilee ya miaka 65 ya upadre, ya paroko wa parokia ya Nkololo, padre Paul Fagan, na kueleza adha wanazozipata wagonjwa pindi wanapohitaji kupatiwa matibabu katika kituo hicho cha afya.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi akizungumza katika jubilee hiyo amesema serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania imeendelea kufanya juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara ili iwe rafiki kwa watumiaji.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa kituo cha afya Songambele Dk.Fidel Felician na baadhi ya wakazi wa Nkololo, Benitha Madulusu na Ngassa Magembe, wanaeleza athari wanazozipata wagonjwa kwa kushindwa kufika kituoni hapo kwa wakati kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.

