Sibuka FM
Sibuka FM
20 May 2025, 5:08 pm

‘‘Vijana ni nguvu kazi ya taifa hili hatupaswi kabisa kuwa tunalalamika kulingana na viongozi wetu ambao tuliwaamini tukawapa kura za kuwa wawakilishi wetu kwenye vyombo vya maamuzi kwa sheria za nchi hii unaruhusiwa kugombea udiwani,ubunge kuanzia miaka 21 hivyo vijana hii ndiyo nafasi yetu pekee ya kufanya maamuzi ya kuwania nafasi za uongozi ili tuwe kwenye vyombo vya kutoa dira ya maendeleo uchaguzi huu tunatarajia kuwaona vijana wakiwania nafasi mbalimbali’’.
Na. Daniel Manyanga
Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) wilayani Maswa mkoani Simiyu wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika October .25 mwaka huu nchini ili wawe sehemu ya kutoa maamuzi na mustakabali wa taifa hili.
Akizungumza katika kikao cha baraza la UVCCM wilayani Maswa, katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Ephraim Kolimba, amewataka vijana hao kuacha kuwa tegemezi na badala yake wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Awali akizungumza katika kikao hicho, mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Maswa Emmanuel Cosmas, amesema kuwa umoja huo upo tayari kuwaunga mkono vijana wote watakaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Kwa upande wao Lucia Christian,Emmanuel Samwel na Catherine Daniel na vijana wa UVCCM wilayani Maswa wameeleza utayari wao wa kushiriki uchanguzi kwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa ngazi ya kata na majimbo kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.

