Sibuka FM
Sibuka FM
3 May 2025, 8:14 pm

‘‘Nani atamfunga Paka kengele? Je nani ambaye ataziona nguvu za wakulima wa zao la pamba wanapohangaika wakati wa kilimo hivi hatuwezi kuwa na soko huria ili kuipa thamani pamba yetu maana naona kabisa vita vya Panzi furaha ya Kunguru anayeumia hapa ni mkulima na siyo mnunuzi kama swala ni soko la dunia basi tuwaruhusu wawekezaji wa viwanda waje nchini ili pamba yetu ilete thamani kwa mkulima ni fikra zangu tu’’.
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi amewataka mameneja na wamiliki wa makampuni yanayonunua pamba mkoani humo kuhakikisha wanazingatia ongezeko la bei ya zao hilo, na kuwalipa wakulima kulingana na bei inavyoongezeka kwa siku husika
Kihongosi ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza katika uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2025/2026 uliofanyika katika mtaa wa Mwakibuga kata ya Nyakabindi wilayani Bariadi na kuagiza wakulima kulipwa kwa kuzingatia ongezeko la bei.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo mkurugenzi mkuu wa bodi ya pamba nchini, Marco Mtunga amewaasa wakulima wa zao la pamba kuhakikisha wanazingatia kanuni bora za kilimo wanazoelekezwa na wataalam wa kilimo ili kuweza kupata mavuno mengi lengo likiwa ni kuweza kumuona mkulima anapata tija katika zao hilo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bariadi ,Simon Simalenga amewataka wakulima kuzingatia ubora wa pamba yao hususan kipindi cha mavuno, huku wakulima wakiomba kuongezwa kwa bei ya zao hilo walau ifike shilingi elfu mbili msimu huu wakieleza kuwa bei iliyotangazwa ni ndogo ikilinganisha na gharama wananzozitumia katika uzalishaji.
Bei ya pamba iliyotangazwa katika uzinduzi huo wa msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2025/2026 ni shilingi 1,150 kwa kilo kwa pamba daraja la kwanza na shilingi 575 kwa kilo kwa pamba daraja la pili, bei ambayo imelalamikiwa na wakulima wa zao hilo mkoani Simiyu wakieleza kuwa haitoshi ikilinganishwa na gharama walizozitumia katika uzalishaji na hivyo kuomba bei iongezwe.
