Sibuka FM

Jela miaka 30, fidia laki mbili kwa kuzini na mwanae wa damu

24 April 2025, 6:40 pm

Muonekano wa nje wa jengo la mahakama ya wilaya ya Maswa ambapo mshtakiwa ,Daud Mussa Mabele amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki mbili kwa kosa la kuzini na maharimu (Mwanaume kujamiana na ndugu yake wa damu) mtoto wake wa kuzaa shauri hilo la jinai lililosimamiwa na mwendesha mashtaka kutoka ofisini ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo, mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm

Nafikiri bado kuna kila sababu kwa mamlaka zilizopewa kutunga sheria kukaa tena chini kuziangalia upya hizi sheria zetu maana haiwezekani kila kukicha matukio ya ukatili wa kinjisia yanatokea licha ya wahusika kuhukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo kama itawezekana adhabu ya kifungo jela ibadilishwe twende kwenye kunyonga hizo ni fikra zangu tu”.

Na, Daniel Manyanga

Mahakama  ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu,Daud Mussa Mabele jina maarufu Lesha  (38) Msukuma ,mkulima mkazi wa kijiji cha Kakola kata ya Shishiyu  kwenda jela miaka 30  na kulipa fidia ya shilingi laki mbili kwa  kosa la  kuzini na maharimu mwenye miaka 14.

Mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa,Mhe.Azizi Khamis,Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi ,Vedastus Wajanga amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe ambayo haikufahamika mwezi September.2024 majira ya usiku huko katika kijiji cha Kakola kata  ya Shishiyu wilayani hapo.

Awali mahakamani hapo ilidaiwa na Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilaya ya Maswa, mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga, kuwa mshtakiwa alizini na maharimu (Mwanaume kujamiana na ndugu yake wa damu) ambaye ni mtoto wake wa kuzaa mwenye umri wa miaka 14 na kumsababishia ujauzito ambapo kitendo hicho kilifanyika baada ya Mama wa Victim kwenda nyumbani kwao kwa ajili ya kujifungua.

Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka  wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga amesema kuwa kosa hilo ni kinyume na  kifungu cha158 (1)(a) cha  sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .

Wajanga amesema kuwa taarifa zilifika kituo cha polisi wilaya ya Maswa ambapo mshtakiwa alikamatwa na alipohojiwa katika kituo hicho  alikataa kabisa kufanya kitendo hicho na baada ya upelelezi kukamilika mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa hatua zingine za kisheria ambapo upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano na kielelezo kimoja ili kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo na baada ya ushahidi huo kutolewa mshtakiwa naye alipewa nafasi ya kuwasilisha utetezi wake ambapo alikili kufanya kitendo hicho na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na anategemewa na familia.

Mara baada ya utetezi huo kukamilika mahakama hiyo ilimtia hatia mshtakiwa, Daud Mussa Mabele jina maarufu Lesha huku mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kumpatia adhabu kali mshtakiwa huyo ili iwe funzo kwake na jamii kwa kuzingatia kuwa kitendo hicho alichokifanya ni kinyume na sheria pamoja na maadili ya Mtanzania na kitendo hicho kimeacha alama isiyoweza kufutika kwa muhanga huku ukizingatia muhanga ameachiwa ujauzito wa miezi saba na ni ukatili wa kijinsia.

Akitoa hukumu hiyo ya jinai kesi Na.6929/2025 iliyotolewa  leo hii mnamo tarehe 24.April.2025  na hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Mhe.Azizi Khamis  mara baada ya kusikiliza utetezi wa pande zote mbili za mshtakiwa na Jamhuri bila kuacha mashaka yoyote ndipo mahakama ikamhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela  pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki mbili kwa muhanga kwa kosa la kuzini na maharimu (mwanaume kujamiana na ndugu yake wa damu) ambaye ni mtoto wake wa kuzaa mwenye umri wa miaka 14.