

9 April 2025, 3:41 pm
“Bado tunakila sababu kwa mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya kujenga kwenye mikondo ya maji maana kila kiongozi yakitokea maafa kama ya mafuriko tunaanza kuwaambia wananchi madhara ya kujenga bondeni Je? Kipindi wanaanza ujenzi mamlaka husika zilikuwa wapi najaribu tu kujiuliza maswali”.
Na, Daniel Manyanga
Zaidi ya kaya 16 zimekosa makazi huku kaya 34 zikiathirika kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha usiku wa kuamkia tarehe 08 ya April mwaka huu wilayani Itilima mkoani Simiyu.
Akizungumza na Sibuka fm mkuu wa wilaya ya Itilima,Anna Gidarya alipofika katika maeneo yaliyiathirika kwa lengo la kujionea na kutoa pole kwa wahanga amesema kuwa changamoto kubwa iliyochangia nyumba ,mazao na mifugo kusombwa ni wananchi baadhi kujenga kwenye mikondo ya maji hivyo kuzuia maji kupita kwa urahisi.
Kufuatia hali hiyo kujitokeza kwa wananchi mwenyekiti wa kitongoji cha Sokoine,Limbu Deus akatoa wito kwa jamii kujenga nyumba bora na imara Ili kuweza kuhimili maji ya mvua.
Wakizungumza kwa simanzi kubwa baadhi ya wananchi waliopatwa na masaibu hayo wameiomba serikali wilayani hapo ione namna bora ya kuwasaidia malazi,chakula na vitu vingine kwa kipindi hichi mara baada ya vitu vyao kusombwa na maji.
Mkuu wa wilaya ya Itilima,Anna Gidarya amesema kuwa tayari timu ya tathimini imeshaanga kazi huku wale ambao hawana makazi akiwataka kuondoka kwenye maeneo hayo na kwenda maeneo salama yaliyotengwa na serikali wilayani hapo.