

19 March 2025, 4:55 pm
‘‘Aliyesema kuwa elimu ni ufunguo wa maisha ni kweli hakukosea ndiyo tunawatu wengi sana ambao hawakuweza kupata elimu ndani ya mfumo rasmi lakini haimaanishi kuwa watu hawa wasiweze kupata fursa ya elimu hata ya ufundi stadi ili kuondoa utegemezi kwenye familia zao’’.
Na,Daniel Manyanga
Imeelezwa kuwa utekelezaji wa mradi wa IPOSA ambao una lengo la kuwafikia na kuwanufaisha vijana wenye umri wa miaka 14 – 19 ambao hawakupata fursa ya elimu kupitia mfumo rasmi mkoani Simiyu utakuwa ni mkombozi kwa vijana hao kwani utawawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali watakazokuwa wakizifanya kutokana na mafunzo watakayoyapata kupitia mradi huo.
Hayo yamesema na katibu tawala msaidizi anayeshughulikia masuala ya uchumi na uzalishaji mkoani Simiyu, Juma Topera wakati akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo ,Kenani Kihongosi wakati wa kufunga mafunzo ya siku 21 ya walimu watakaokuwa wakiwafundisha vijana hao fani mbalimbali kupitia mradi huo wa IPOSA, na kueleza namna ambavyo mradi huo ni muhimu kwa vijana wa mkoa wa Simiyu.
Awali akitoa taarifa juu ya mafunzo hayo mkufunzi mkazi kutoka taasisi ya watu wazima mkoa wa Simiyu, Chago Igoloka, amesema kuwa mradi unalenga kuwawezesha vijana hao ili wasiachwe bila msaada wa kielimu huku mhadhiri msaidizi kutoka taasisi ya elimu ya watu wazima, Rose Mgaya akieleza kilichowasukuma kuanzisha mradi huo kwa ajili ya kuwasaidia vijana ambao hawajapata elimu katika mfumo rasmi wa serikali.
Alfred Thobias, Mary Manfred na Noel Mlunde ni baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ya siku 21 wameeleza namna ambavyo yatasaidia kuwakwamua kiuchumi vijana waliolengwa kufikiwa na mradi huo.