

14 February 2025, 4:55 pm
“Hatuwezi kuendelea kuona wakulima wanakosa thamani pindi wanapouza mazao yao wakati wanahangaika kulima alikuwa mwenyewe bila ya usaidizi wowote wa wanunuzi”.
Na, Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoni Simiyu Aswege Kaminyoge amesema kuwa serikali ya wilaya hiyo haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaouza na kununua mazao ya nafaka mchanganyiko pasipo kufuata mfumo wa stakabadhi ghalani kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na maelekezo ya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Mkuu huyo wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge ametoa rai hiyo wakati akizungumza katika ufunguzi wa ununuzi na uuzaji wa mazao mchanganyiko kupitia stakabadhi ghalani wilayani humo na kuwataka watu wote kuzingatia maelekezo ya serikali ili kuleta thamani na tija kwa wakulima.
Godfery Mpepo ni mrajis msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Simiyu, amewataka viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) mkoani hapo kuwaelimisha wakulima juu ya umuhimu wa matumizi ya mfumo huo.
Akizungumza katika ufunguzi wa msimu wa ununuzi na uuzaji wa mazao mchanganyiko,Cosmas Budodi afisa ushirika wilaya ya Maswa amewataka watendaji wa vijiji kuhakikisha wanafika katika vituo vya kununulia na kuuzia Ili kukagua mizani inayotumika lengo ni kuondokana na wakulima kuibiwa pindi wanapouza.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa AMCOS, wakulima na wanunuzi wa mazao hayo wameeleza faida za matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani.
Jumla ya tani 90 za mazao mchanganyiko zimeuzwa kupitia mnada uliofanyika katika ufunguzi huo wa uuzaji wa mazao hayo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, ambapo kilo moja imenunuliwa kwa shilingi 1,370 na hivyo tani hizo zimeuzwa kwa jumla ya kiasi Cha shilingi milioni 123,300,000