Sibuka FM

Itilima: Mwalimu mkuu jela miaka 3 kwa udanganyifu wa mtihani

10 February 2025, 6:30 pm

Muonekano wa jengo la mahakama ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu ambapo imefanyika hukumu ya mwalimu mkuu Picha ni kutoka maktaba ya Sibuka fm

Kama taifa limeweka kuwepo na mitihani ya kupima uwezo wa uelewa kwa wanafunzi juu ya kile wanachofundishwa na walimu shuleni sasa inatoka wapi tena nguvu ya walimu kuwasaidia wanafunzi hatuoni kwamba tunatengeneza taifa la wanafunzi tegemezi wa akili”.

Na, Daniel Manyanga

Mahakama ya wilaya ya Itilima imemhukumu Bahati Suguti ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Sunzula B iliyopo wilayani itilima mkoani Simiyu kifungo cha miaka mitatu jela kwa makosa mawili huku wenzake watano wakiachiwa huru.

Washitakiwa hao jumla walikuwa sita ambao ni walimu na walishitakiwa katika mahakama ya wilaya ya Itilima kwa makosa mawili kosa la kwanza ni la kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .

Kosa la pili la ni kusaidia wanafunzi kutenda kosa la udanganyifu kinyume na kifungu cha 23 na 24 vya sheria ya baraza la taifa la mitihani sura ya 107 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2019 vikisomwa pamoja na kanuni ya 16(11)(c) ya kanuni za mitihani ya mwaka 2016 kama ilivyo tangazwa kwenye gazeti la serikali namba 89 la mwaka 2016.

Awali Mahakamani hapo , ilidaiwa na mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka wilaya ya Itilima ambaye ni mkaguzi msaidizi wa polisi Jaston Mhule kuwa mnamo Oktoba 25, 2023 na Oktoba 26, 2023 katika shule ya msingi sunzula B ndani ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu washitakiwa mwalimu mkuu wa shule hiyo Bahati Suguti, Stephano Daudi, Fauzia David, Mwita Boniface ,Masatu Jepharine na Salome Aron walikula njama ya kutenda kosa la kusaidia wanafunzi wa darasa la nne kutenda kosa la udanganyifu katika vyumba vya mtihani.

Oktoba 25 na 26, 2023 mtihani wa upimaji ya darasa la nne ukiwa unaendelea washtakiwa waliwasaidia wanafunzi wa darasa la nne kutenda kosa la udanganyifu katika vyumba vya mtihani.

Taarifa zilifika kituo cha polisi baada ya kubainika katika kipindi cha usahishaji wa mtihani ambapo washtakiwa walikamatwa na kuhojiwa kuhusiana na kosa hilo na baada ya upelelezi kukamilika washtakiwa walifikishwa mahakamani.

Kesi hiyo imesikilizwa katika mahakama hiyo chini ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Itilima ,Mhe.Roberth Kaanwa upande wa mashtaka ulikuwa na jumla ya mashahidi 09 na vielelezo 04 na upande wa watuhumiwa walijitetea bila kuwa na mashahidi baada ya ushahidi wa upande wa mashitaka kutolewa mahakama iliwapa nafasi washtakiwa walijitetea na walikana kuhusika na makosa hayo.

Akitoa hukumu ya shauri la jinai Na.27062/2024 katika mahakama ya wilaya ya Itilima hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo,Mhe. Roberth Kaanwa amesema kutokana na ushahidi na vielelezo uliowasilishwa mahakamani,mahakama imejiridhisha pasina shaka mwalimu mkuu wa shule hiyo Bahati Suguti amehusika moja kwa moja na kosa la kusaidia wanafunzi wa darasa la nne kutenda kosa la udanganyifu katika vyumba vya mtihani huku wenzake wakiachiwa huru.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa kwa kosa la kwanza la kula njama ya kutenda kosa mahakama aliwaachia huru watuhumiwa wote sita kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuithibitishia mahakama hiyo kuwa walitenda kosa.

Kwa upande wa kosa la pili la kusaidia wanafunzi kutenda kosa la udanganyifu mahakama iliwaachia huru washitakiwa watano kutokana na ushahidi wa upande wa mashitaka kutowataja wahusika hao na badala yake ushahidi ulimlenga moja kwa moja mshitakiwa namba moja ambaye ni mwalimu mkuu wa shule hiyo Bahati Suguti hatua iliyopelekea mahakama ya wilaya ya hiyo kumtia hatiani mshitakiwa namba moja Bahati Suguti na kuwaachia huru washtakiwa 05 .

Baada ya kutiwa hatiani upande wa mashtaka uliomba mshitakiwa apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa jamii kwani tukio hilo linamadhara makubwa kwa jamii na serikali inatumia gharama kubwa kuratibu zoezi la mitihani lakini pia kukiwa na udanganyifu katika mtihani kunapelekea kupata watalam ambao hawatoi mchango chanya katika ujenzi wa taifa.

Mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na ana familia inayomtegemea na ni mtumishi wa serikali.

Na ndipo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya hiyo,Mhe. Roberth Kaanwa alimhukumu adhabu ya kwenda jela kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi milioni tano baada ya kushindwa kulipa faini mwalimu huyo ameenda gerezani.