

4 February 2025, 11:19 am
‘‘Hivi hatuwezi kumaliza migogoro ya ardhi,mirathi na ndoa kwenye jamii zetu sheria zinasemaje kwa mtu ambaye atafanya kesi za aina kama hiyo kama changamoto ni sheria zetu basi tuziboreshe na kama ni elimu ndogo ya kisheria kwa wananchi wetu vyombo vinavyohusika kutoa elimu wanajukumu kubwa la kumaliza migogoro hiyo’’.
Na, Paul Yohana
Migogoro ya ardhi,mirathi na ndoa imetajwa ni kesi zinazoongoza kulipotiwa katika mahakama za wilaya ya Maswa mkoani Simiyu hali ambayo inachangiwa na uelewa mdogo wa maswala ya kisheria kwa wananchi wanaoshtakiana kwenye vyombo vya sheria.
Hayo yamesemwa na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya Maswa,Mhe.Enos Missana wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria nchini ambapo kwa wilaya ya Maswa yamefanyika kwenye viwanja vya mahakama na kuhudhuriwa na wadau wa mahakama.
Missana amesema kuwa kutokana na uchunguzi uliofanywa katika wiki wa sheria wamebaini kuwa asilimia kubwa ya wananchi hawana uelewa wa maswala ya kisheria hivyo kuchangia migogoro mingi ambayo wakati mwingine ingeweza kumalizikia huko nyumbani bila hata ya kufika katika vyombo vya sheria.
Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Maswa,Mhe.Enos Missana ameongeza kuwa mahakama itahakikisha elimu hii inaendelea kutolewa hata baada ya maadhimisho ya wiki ya sheria nchini pamoja kuanzishwa kwa klabu mbalimbali na kushirikisha wadua wa mahakama katika kutoa elimu kwa wananchi juu maswala ya kisheria ili kupunguza migogoro kwa jamii.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa wilaya ya Maswa ,Aswege Kaminyoge amewaomba wananchi kushirikiana na mahakama na vyombo vingine vya dola ili kuhakikisha elimu ya maswala ya kisheria inamfikia kila mwananchi hali ambayo itapunguza migogoro kwenye jamii zetu.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria maadhimisho wamesema kuwa elimu ndogo ya kisheria juu ya maswala ya ardhi , mirathi na ndoa ndiyo imekuwa janga kubwa la mauwaji mbalimbali kwa wananchi yanayotokea hivyo elimu itolewe bila kuwa na ukomo na hii itasaidia kupunguza migogoro kwenye jamii zetu.