Rais Samia apeleka furaha kwa yatima mkoani Simiyu
31 December 2024, 9:06 pm
“Dini ya kweli ni kuwakumbuka wenye uhitaji ili nao waweze kujisikia kuwa wanathaminiwa na jamii na kuwatambua katika kuijenga nchi bila kujali mapungufu waliyonayo”.
Na, Daniel Manyanga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, amewakumbuka watoto yatima Mkoani Simiyu katika kusherekea Sikukuu ya mwaka mpya 2025 kwa kuwazawadia zawadi mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi ,Simon Simalenga amekabidhi zawadi hizo za sikukuu kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Simiyu ,Kenan Kihongosi katika kituo cha kulelea yatima cha Mayega Wilayani Busega.
Zawadi zilizokabidhiwa ni pamoja na Sukari Kilo 20,Unga wa Sembe Kilo 50, Mchele Kilo 50,Mbuzi wanne, Mafuta ya kupikia Lita 10,Mifuko mitatu ya Sabuni za unga,pamoja na Katoni 10 za Juice
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo za sikukuu kituoni hapo,Simon Simalenga ameikumbusha jamii mkoani Simiyu kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama hususan jeshi la Polisi Ili kuwalinda watoto dhidi ya ukatili unaoendelea kutokea kwa watoto.
Amesema watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu hivyo ni jukumu la wazazi kwa pamoja kuwalea watoto pamoja na kuzingatia suala la ulinzi na usalama wao.
Zawadi za Mhe.Dkt.Samia zinakabidhiwa kwa watoto yatima katika kituo cha Mayega wilayani Busega ili kuwezesha Watoto hao kufurahia kwa pamoja katika kusherehekea Sikukuu ya mwaka mpya 2025.