Wazazi wafelisha wanafunzi 213 elimu ya msingi mkoani Simiyu
23 December 2024, 8:36 pm
“Pamoja na kwamba maandiko matakatifu yanasema kuwa mkamate sana elimu usimwache aende zake mshike maana yeye ni uzima wako Mithali 4:13 lakini wazazi wameendelea kuwa vikwazo kwa wanafunzi kutimiza ndoto zao”.
Na, Daniel Manyanga
Wanafunzi 213 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka wa masomo 2024 waliandika majibu siyo sahihi ili kufeli mtihani wa taifa kulingana na maagizo ya wazazi wao ya kuandika majibu yasiyo sahihi hivyo kuchangia kushuka kwa ufaulu kutoka asilimia 80.12 hadi asilimia 76.01 katika watahiniwa 38171 na kufaulu 29012 mkoani Simiyu.
Akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri mkoa wa Simiyu (RCC), Khalifa Shemahonge afisa elimu mkoa huo amesema kuwa walifanya utafiti kwa wanafunzi 255 ambao walikuwa wanafanya vizuri katika mitihani ya ndani ya mkoa lakini katika mtihani wa taifa waliweza kufeli licha ya kuwa na uwezo kufaulu.
Wakizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri mkoa wa Simiyu,Njalu Silanga mbunge wa jimbo la Itilima na Leah Komanya mbunge wa jimbo la Meatu walihoji kwa nini ufaulu umeshuka katika kipindi cha miaka minne licha ya kuweka miundombinu rafiki ya kupandisha ufaulu mkoani hapo ikiwemo kuanzishwa kwa makambi kwa madarasa ya mitihani.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi akatoa maagizo kwa katibu tawala mkoa huo,Prisca Kayombo ya kuwaandika barua idara ya elimu ya kueleza kwa nini ufaulu umeshuka ili hatua sitahiki ziweze kuchukuliwa.