DC Kaminyoge aongoza wananchi wa Isageng’he kupanda miti
10 December 2024, 12:15 pm
“Tanzania siyo kisiwa hivyo hatuwezi kujitenga katika vita ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama ambavyo dunia inataka ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia na upandaji wa miti”.
Na, Nicholaus Machunda
Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na jangwa jumla ya miti milioni moja na laki tano inatarajiwa kupandwa wilayani Maswa mkoani Simiyu ili kurudisha uoto wa asili katika maeneo yaliyopoteza uoto ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kupanda idadi ya miti hiyo kwenye kuadhimisha miaka 63 ya uhuru.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isageng’he kata ya Sukuma mkuu wa wilaya ya Maswa ,Aswege Kaminyoge wakati wa zoezi la upandaji wa miti amesema kuwa umuhimu wa zoezi hilo ni kurudisha uoto wa asili katika maeneo ambayo yameshapoteza uoto wa asili ikiwa na lengo la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Aswege Kaminyoge ameelekeza kuwa miche ya miti igawiwe bure kwa Wananchi na taasisi ili waweze kupanda miti na kufikia lengo la kupanda miti zaidi ya milioni moja na laki tano kwa mwaka huu 2024/ 2025 kama maelekezo ya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Duttu Lubinza ni afisa maliasili na mazingira halmashauri ya wilaya ya Maswa amesema kuwa halmashauri inamkakati wa kuhakikisha wanasambaza miti kila maeneo ili kurahisisha upatikanaji wa miche ya miti hiyo.
Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Isageng’he waliojitokeza kushiriki zoezi la upandaji wa miti wameshukuru uongozi wa wilaya kwa kuhamasisha zoezi hilo huku wakiahidi kuitunza ili isiharibiwe na Mifugo.