TAWA yavuna Viboko wawili na kutoa kitoweo kwa wananchi Busega
20 November 2024, 8:43 pm
“Usalama wa raia ni ajenda ya kwanza katika Taifa lolote hatuwezi kuzungumzia maendeleo wakati huo raia wake wanapitia changamoto za kiusalama wao na mazao hasa waishio kandokando ya mapori au hifadhi.”
Na, Daniel Manyanga
Viboko wawili waliokuwa wanahatarisha usalama wa wananchi na mali zao kwenye kata ya Kabita wilayani Busega mkoani Simiyu wameuliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) ikiwa ni zoezi la uvunaji la wanyama hatarishi katika jamii.
Ng’oga Genda na Rahel Nicholaus wakazi wa Kabita wakizungumza na Sibuka fm wameomba zoezi hilo liwe endelevu ili waweze kufanya shughuli zao ikiwemo kilimo bila hofu yoyote ya wanyama hatari wanaokwamisha utendaji wa shughuli za kiuchumi kwa kuhofia usalama wao na mazao yao.
Michael Mabula ni mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM kata ya Kabita ameipa kongole serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori (TAWA) kwa hatua hiyo ya kupunguza wanyama walio hatari.
Akizungumzia ufanikishaji wa zoezi hilo afisa wanyamapori mwandamizi wa mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori (TAWA) pori la akiba la Kijereshi,Rogathe Wado amesema kuwa uvunaji wa wanyama wanaohatarisha maisha na mali za watu utakuwa endelevu.