RC Kihongosi amwaga fedha kwa bodaboda wa Nyashimo Busega
18 September 2024, 4:55 pm
“Mchango wa maendeleo na kupunguza wimbi la ajira umekuwa mkubwa sana kwa Taifa kutokana na baadhi ya vijana kujiajiri wao wenyewe kupitia bodaboda hivyo kujiongezea kipato“.
Na, Daniel Manyanga
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenani Kihongosi ametoa kiasi cha fedha milioni moja kwa maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda wanaofanya kazi zao katika eneo la Nyashimo ambapo ni makao makuu ya wilaya ya Busega ili kusaidia ujenzi wa kibanda cha kuegesha pikipiki wakati wakisubiri abiria.
Kihongosi ametoa kiasi hicho cha fedha wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Nyashimo wilayani hapo.
Kenani Kihongosi amesema kuwa fedha hiyo ni mchango wake wa kutambua uhitaji mkubwa na muhimu kwa maafisa usafirishaji hao kulingana na kazi wanayoifanya ya kujiongezea kipato Cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kihongosi ameongeza kuwa fedha hiyo ikatumike kwenye lengo mama lililokusudiwa na siyo vinginevyo huku akimtaka afisa maendeleo ya jamii wilayani hapo kuwasimamia maafisa usafirishaji hao namna ya kuwa na katiba,kusajili kikundi na kufungua akaunti bank ili kikundi hicho kiweze kutambulika.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wamepongeza juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe,Dkt.Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali lakini likaibuka swala la mradi wa kilimo cha Miwa kutokana na baadhi wa wananchi kutokushirikishwa juu ya ujio wa mradi huo.