Bariadi:Wanandoa waathirika wa Ukimwi wapata mtoto asiye na maambukizi
10 July 2024, 3:59 pm
“Kupata ukimwi siyo mwisho wa maisha na wala siyo kiama vijana wawili wilayani Bariadi wa jinsia ya kiume na kike ambao ni waathirika wa ukimwi wamezaa mtoto ambaye hana virusi vya ukimwi’’
Na,Daniel Manyanga
Watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wilayani Bariadi mkoani Simiyu wameiomba serikali na wadau wa masuala ya afya kuendelea kutekeleza afua za Ukimwi ambazo hapo awali zilikuwa zikiwakutanisha pamoja na kuwasaidia kujiamini na kuendelea kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo pasipo kukata tamaa.
Akizungumza na Sibuka Fm mjini Bariadi, James Nyamoye ambaye ni kijana mwenye umri wa miaka 29 anayeishi na virusi vya Ukimwi alivyozaliwa navyo, ameeleza namna ambavyo kambi zilizokuwa zikiwakuatanisha pamoja zilikuwa zinawasaidia kutokata tamaa kutumia dawa za kufubaza na kuondoa unyanyapaa kwa jamii wanayoishi.
Mary James ni mke wa James Nyamoye ambaye anaeleza namna alivyoweza kuzingatia maelekezo aliyopewa na wataalam wa afya katika kambi zilizokuwa zikiwakutanisha watu wenye VVU na kumuwezesha kupata watoto wawili ambao hawana maambukizi.
Kwa upande wao ndugu wa watu wenye maambukizi ya VVU wameeleza namna ambavyo makongamano yaliyokuwepo awali ambayo yaliwakutanisha vijana wenye maambukizi kutoka maeneo mbalimbali yalivyowasaidia kukabiliana na VVU.
Akitolea ufafanuzi suala la hilo mratibu wa kuthibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, homa ya Ini pamoja na magonjwa ya ngono mkoa wa Simiyu Dk. Khamis Kulemba ameeleza jitihada zinazofanywa ili kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanapata huduma stahiki.