Sibuka FM

RUWASA wilayani Maswa kutumia billion 3.7 kumtua mama ndoo kichwani

26 June 2024, 9:38 am

Pichani ni meneja RUWASA wilaya ya Maswa , Mhandisi Lucas Madaha aliyesimama , upande wa kulia aliyekaa ni mwenyekiti wa halmashauri,Paul Maige mwenye kaunda suti dark bluu Picha na Nicholaus Machunda

Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya vijijini utaongeza uchumi wa familia kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta maji hivyo watajikita katika shughuli za kimaendeleo.”

Na, Daniel Manyanga

Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA wilayani Maswa mkoani Simiyu imepanga kutumia kiasi cha billion 3.7 kwa mwaka fedha 2024/25 ili kutimiza adhima ya serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndoo kichwani.

Hayo yamesemwa na meneja RUWASA wilayani hapo, Mhandisi Lucas Madaha wakati wa kikao cha wadau wa maji kilichokuwa kikijadili namna ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama hasa vijiji ambavyo havijapata huduma hiyo kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa na kuhudhuriwa na wadau wa maji.

Mhandisi Madaha amesema kuwa katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama RUWASA imepanga kutumia kiasi cha billion 3.7 katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji kwenye maeneo ambayo yanachangamoto ya huduma hiyo pamoja kukamilisha miradi ambayo haijakamilika kwa mwaka huu wa fedha unaoishia June 30 ili kutimiza adhima ya serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndoo kichwani.

Sauti ya meneja RUWASA mhandisi Lucas Madaha akizungumzia bajeti ya maji kwa mwaka ujao wa fedha.

Awali akifungua kikao hicho cha wadau wa maji mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi wilayani hapo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya maji ili kuwaondolea adha wananchi wa wilaya hiyo kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.

Aswege Kaminyoge amesema kuwa serikali ya awamu ya sita kupitia RUWASA wilayani hapo imetenga kiasi cha million 200 ili kufanya utafiti wa maji ya chini kwa vijiji ambavyo vinachangamoto hiyo ili wananchi katika maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama wakati wanasubiri mradi mkubwa wa maji ya ziwa Victoria utakao gharimu zaidi ya billion 400.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akizungumza kwenye kikao hicho

Nao baadhi ya wadau na watumiaji wa huduma ya maji waliohudhuria kikao hicho wameomba RUWASA kuwa wawazi kwenye vigezo vinavyotumika ili kubaini changamoto ya maji katika maeneo yao kutokana na kuwepo kwa maeneo yenye changamoto ya maji kwa muda mrefu lakini bado hayajapata huduma hiyo.

Sauti ya wadau wa maji wakiomba kuboreshwa kwa huduma za maji
Picha mbalimbali zikionesha wadau wa maji wakifuatilia mijadala inayoendelea kwenye kikao hicho Picha na Nicholaus Machunda