Sibuka FM

Wawili wafariki kwa ugonjwa wa kuhara, kutapika Maswa

21 May 2024, 12:34 pm

Pichani ni mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akizungumza na wananchi kijijini hapo Picha ni kutoka maktaba ya Sibuka Fm

Usafi siyo kuvaa nguo nzuri tu bali usafi ni kuwa na choo kizuri ambapo kinakufanya uweze kuwa salama na magonjwa ya  mlipuko leo hii kesi nyingi za kuhara na kutapika ni kukosa vyoo sasa hatutawavumilia wale wasiokuwa na vyoo.

Na, Daniel Manyanga 

Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Aswege Kaminyoge amewaagiza mkurugenzi mtendaji, afisa afya na afisa tarafa kufanya msako wa nyumba kwa nyuma  ambazo hazina vyoo, kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yakiwemo kuhara na kutapika wilayani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Aswege Kaminyoge amesema kuwa msako huo unakuja kufuatia kuwepo kwa vifo vya watu wawili katika kijiji cha Mandang’ombe kata ya Mbaragane huku vifo hivyo vikitajwa kutokana na ugonjwa wa kuhara na kutapika.

Kaminyoge amesema kuwa msako huo wa nyumba kwa nyumba unalenga kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yanatokea hapa nchini huku kaya zitakazobainika hawana vyoo wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua kali kwa mjibu wa sheria za nchi.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akitoa maagizo kwa watendaji

Aswege Kaminyoge ameongeza kuwa  mama mwenye umri wa miaka 80 na kijana wa miaka 27 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa kuhara na kutapika kwa kile kilichotajwa kutokuwa na vyoo huku wengine wanne wakiwa wamelazwa katika kituo cha afya cha Lalago katika kata ya Lalago wakipatiwa matibabu zaidi.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Maswa

Kwa upande wake kaka wa marehemu, Charles Francis na babu wa marehemu Maku Machame Wamesema kuwa mnamo majira ya sita usiku marehemu walianza kutapika na kuhara ambapo walifanikiwa kuwapeleka katika kituo cha afya cha Lalago kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na kula chakula walipokuwa wakifanya kibarua cha kupukuchuwa mahindi.

Sauti za baadhi ya ndugu wa marehemu

Awali afisa afya wa halmashauri ya wilaya ya Maswa Salima Mahizi amesema kuwa tayari halmashauri imeshachukua hatua ili kukabiliana na changamoto hiyo iliyojitokeza katika maeneo hayo.

Sauti ya afisa afya akizungumzia hatua ambazo zichukuliwe na wananchi