Mikopo umiza ni ugonjwa mwingine kwa watumishi wa umma Simiyu
3 May 2024, 3:58 pm
Ubunifu wa kufanya kazi nyingine tofauti ile ambayo umeajiriwa ni njia pekee inayoweza kuwakomboa watumishi wa umma na kuondokana na mikopo umiza ambao ni ugonjwa mwingine hatari.
Na,Daniel Manyanga
Kaimu mkuu wa mkoa wa Simiyu Bi.Anna Gidarya amewataka watumishi wa umma kuacha kujishughulisha na mikopo umiza wanayokopa kutoka kwenye taasisi mbalimbali hali ambayo imewafanya wengine kuwa na umasiki hivyo kuondoa heshima na jina la mtumishi wa umma.
Bi.Anna Gidarya ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa umma wa kada mbalimbali mkoani hapo ambapo amesema kuwa kumekuwepo na malalamiko ambayo wamekuwa wanayapokea kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kutoka kwa watumishi kujiingiza kwenye mikopo umiza ambapo wapo wengine hadi kadi za benki zinashikiliwa na taasisi zinazokopesha mikopo umiza.
Gidarya amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za watumishi wa umma ili kuleta usawa na ustawi kuanzia ngazi za chini na kuongeza kuwa wakuu wa idara wasimamie na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato katika wilaya zote mkoani hapo.
Kwa upande wake katibu tawala mkoa wa Simiyu Bi.Prisca Kayombo amesema kuwa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kama mwajiri imeendelea kuweka mazingira mazuri na rafiki hasa ya kiutendaji kwa kuendelea kuongeza vitendea kazi na kujali maslahi ya watumishi wa umma mkoani hapo.