RC Nawanda toeni maji bure kwenye maeneo yaliyoathirika na magojwa ya mlipuko
12 January 2024, 10:21 am
Huduma za Maji Safi na Salama zinazotolewa na Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira mjini Maswa(MAUWASA) na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) zitolewe bure kwa wananchi katika maeneo yaliyoathirika na mlipuko.
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda ameitaka mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (MAUWASA) na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) Wilayani Maswa kutoa huduma ya maji Safi na Salama bure katika maeneo yaliyoathirika zaidi na magonjwa ya mlipuko ya Kuhara na kutapika.
Dkt.Nawanda ametoa maagizo hayo wakati wa kikao kazi cha kukabiliana na kupambana kuenea kwa magojwa hayo kilichowakutanisha Watendaji Kata na Kijiji,Maafisa afya,Wazee Maarufu na Viongozi wa Dini kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo kikiwa na lengo la kuhamasisha usafi wa mazingira ili kujikinga magonjwa ya milipuko wilayani hapo.
Dkt.Nawanda ameongeza kuwa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Maswa,Watendaji wa kata na Wakuu wa idara wahakikishe wanafanya ukaguzi wa usafi wa nyumba kwa nyumba pamoja na kuhakikisha hakuna watu wanaofanya biashara ya vyakula mashuleni,stund za mabasi na wauzaji wa pombe kwenye virabu kuwe na vyoo safi na maji safi na salama na kama hakuna vitu hivyo basi virabu hivyo vifungwe mara moja.
Wakitoa taarifa ya utekeleza wa mikakati waliyojiwekea toka kuripotiwa kwa magonjwa ya mlipuko wilayani hapo mbele ya mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda baadhi ya watendaji wa kata wamesema kuwa wanaendelea kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi ikiwemo na kuwapiga faini kaya ambazo zinabainika kutokuwa nyoo.