RC Nawanda apiga marufuku uuzaji wa vyakula mashuleni Simiyu
9 January 2024, 1:17 pm
Marufuku uuzaji wa vyakula mashuleni pamoja na kula vyakula maeneo yenye mikusanyiko ya watu ili kujikinga na kuenea kwa mlipuko wa magonjwa ya Kuhara na Kutapika.
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Dkt.Yahaya Nawanda amepiga marufuku uuzaji wa vyakula mashuleni pamoja na ulaji wa vyakula vya msibani lengo ni kupambana na kukabiliana kuenea kwa magonjwa ya mlipuko mkoani hapo ikiwemo Kipindupindu.
Marufuku hiyo imekuja kutokana na kuwepo kwa kesi za watu kufariki na wengine kuuguwa ugonjwa wa Kutapika na Kuhara mkoani hapo hali ambayo imepelekea kufungwa kwa baadhi ya shughuli za kijamii ikiwemo minada inayokusanya watu wengi hali ambayo inaweza kusababisha watu kuweza kuambukizwa magonjwa hayo.
Dkt.Nawanda akizungumza na Watendaji,Maafisa afya na Wananchi kwa nyakati tofauti tofauti mkoani hapa amesema kuwa hataki kusikia kesi za watu wamepata magonjwa ya mlipuko mkoani hapo hali ya kwamba kuna njia za kuzuia kuenea kwa magonjwa hayo ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu mkoani hapa.
Katika hatua nyingine Dkt.Nawanda amewataka Watendaji wote na Maafisa afya kufanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba ili kubaini nyumba ambazo hazina vyoo na kaya ambazo zikipatikana hazina vyoo faini yake ni shilingi 50,000/=