Pangani FM

Bima ya Afya CHF: Wigo umeongezwa sasa huduma hadi nje ya Halmashauri.

21 January 2021, 2:51 pm

Wananchi wamehimizwa kujiunga kwa wingi katika Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii CHF iliyoboreshwa ili wapate vitambulisho vitakavyowasaidia kupata matibabu kwa mwaka mzima katika vituo vya kutolea huduma za Afya ikiwemo na Hospitali za Rufaa.

Hayo yamesemwa leo na Mratibu wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii Wilayani Pangani Bwana Ramadhani Kimomwe wakati akizungumza na Pangani FM, ambapo amesema kuwa Mfuko huo umekuja mahususi kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya tofauti na ilivyokuwa awali.

“Kwa sasa zile huduma ambazo tulikuwa tunapata awali zimeboreshwa zaidi, awali ilikuwa kupitia CHF unapata huduma kwa ngazi ya Halmashauri tu lakini kwa sasa unapata huduma zote katika Mkoa wa Tanga na nje ya Mkoa wa Tanga”. Pia tumeongeza wigo wa huduma  kwa kipindi cha Mwaka mzima kwa Mwanachama kuchangia Shilingi 30,000. .  

Amesema Bwana Kimomwe

Bwana Kimomwe amesema kuwa kwa sasa Wananchi wanaweza kujiunga na CHF iliyoboreshwa kwenye Ofisi zao za Vijiji, na kuanza kupata huduma za Afya kama Mwanachama mara baada ya kujiunga na Mfuko huo.

“Nendeni katika Ofisi zenu za Vijiji mkajiunge na CHF iliyoboreshwa, watendaji wenu wa vijiji wamepewa mafunzo na wanajua taratibu zote kujiunga ni rahisi sana”. “Sasa hivi tumeboresha sana mana ukishaingizwa tu kwenye mfumo wewe utafahamika kama Mwanachama wa CHF iliyoboreshwa na unaweza kuanza kupata huduma kama Mwanachama hapo hapo hii ni tofauti na awali ilikuwa usubirie hadi mwezi mmoja upite”.

Amesisitiza Mratibu wa CHF iliyoboreshwa Pangani na kuongeza kuwa “Mfuko huo hadi sasa umeshawanufaisha Wananchi wengi, huku akiimba jamii kuchangamkia fursa ya kujiunga na Mfuko huo ili kuwa na uhakika wa Matibabu kwa Mwaka mzima.

“Wale ambao mmemaliza muda wenu utaratibu ni huo huo pia mfike kwenye Ofisi zenu za Vijiji ili muendelee kupata Huduma za Afya kwa uhakika”.  

Amesema Bwana Ramadhani Kimomwe.

Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii CHF iliyoboreshwa ni Mpango muhimu wa hiari ulioanzishwa kwaSheria Na. 1 ya mwaka 2001 (Sura ya 409 ya Sheria za Tanzania Toleo la 2002) wa kaya, kikundi au familia au mtu binafsi kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua, ambapo Wanachama wanapata huduma bora ya afya kwa kipindi cha mwaka mzima.