Mkuu wa wilaya ya Maswa ,Aswege Kminyoge amezitaka taasisi zote za serikali wilayani hapo kupanda miti.
12 January 2023, 4:31 pm
Na mwandishi wetu,Daniel Manyanga.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ameziagiza taasisi zote za serikali wilayani hapo kuhakikisha zinatenga bajeti ya utunzaji wa mazingira wakati wa uandaaji wa bajeti kuu ya serikali kwa mwaka fedha 2023/2024 ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na utunzaji wa chanzo kikuu cha maji cha bwawa la New Sola ambao ni mto Sola.
Aswege Kaminyoge ameyasema hayo wakati wa zoezi la upandaji miti katika bonde la mto Sola ambalo ndiyo chanzo kikuu cha maji katika bwawa la New Sola linalohudumia wakazi wa mji wa Maswa pamoja na vijiji kumi na mbili vinavyozunguka bwawa hilo katika matumizi mbalimbali ya kibinadamu.
“Taasisi zote za serikali zipewe eneo la kupanda miti katika bonde hii na kuhakikisha wanalitunza eneo hilo, kila taasisi ihakikishe inatenga bajeti ya utunzaji wa mazingira ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, lakini baraza la madiwani kwa robo mwaka huu lazima katika vikao vyenu muweze kujadili suala la utunzaji wa mazingira katika bonde hili” amesema mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge.
“Afisa mazingira na watendaji wa vijiji vinavyozunguka bonde la mto Sola hakikisheni hakuna shughuli za kibinadamu zozote zinazofanyika ndani ya mita 60 katika bonde hili ikitokea nikakuta mtu anafanya shughuli za kibinadamu mimi nitakukamata wewe afisa mazingira na mtendaji na kukuweka ndani masaa 48 maana haiwezekani shughuli za kilimo zinafanyika halafu wewe upo na unaona lakini huchukui hatua zozote” amesema Aswege Kaminyoge.
“Ni sheria afisa ardhi yeyote anayegawa kiwanja kwa wananchi ahakikishe kiwanjani hapo anapanda miti, maafisa ardhi na mipango nendeni mukalisimamia hili maana ukweli usiopingika kila mwananchi mwenye kiwanja hawajapanda miti” amesema Aswege Kaminyoge.