Sibuka FM
Sibuka FM
11 April 2026, 5:52 am

“Wakati taarifa kutoka dawati la jinsia na watoto zikieleza kuwa idadi kubwa ya watu wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ni wanawake na watoto, lakini hali ni tofauti kwa baadhi ya wanaume wa mkoa wa Simiyu wameeleza wamekuwa wakipitia ukatili kutoka kwa wake zao, na kwamba mambo yanakuwa magumu zaidi kwao kutokana na kukosa msaada wa haraka pindi wanapofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili”.
Na,Daniel Manyanga
Wanaume wanaofanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia na wake zao ikiwemo vipigo mkoani Simiyu, wameiomba serikali kupitia jeshi la polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto kuwasaidia pindi wanapofika katika ofisi hizo ili waweze kuondokana na vitendo hivyo ambavyo wamekuwa wakifanyiwa na wake zao mara kwa mara pasipokuwa na msaada.
Wakizungumza na Sibuka Fm, Mashaka Magembe,Sayi Nkilila na Daniel Sitta wamesema kuwa wamekuwa wakikutana na vikwazo pindi wanapofika katika kituo cha polisi kitengo cha dawati la jinsia kwa ajili ya kupata msaada juu ya ukatili wanaoupata kutoka kwa wake zao ambapo badala ya kupatiwa msaada wamekuwa wakiambulia kejeli na kubezwa na maafisa jeshi hilo.
Juma Mashauri ni mwenyekiti wa mtaa wa Nyamhimbi, uliopo kata ya Somanda hapa anakiri kuwepo kwa matukio ya wanaume kupigwa na wake zao na amekuwa akizipokea kesi hizo kwa nyakati tofauti tofauti.
Kwa upande wake mkuu wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Simiyu,Inspekta Dionice Katemana amekiri kupokea taarifa za ukatili kwa wanaume dhidi ya wake zao japo kuwa ni kwa idadi ndogo huku akikanusha kitendo cha kuwakejeli na kuwabeza wanaume wanapoenda kuripoti kufanyiwa ukatili na wake zao.