Sibuka FM
Sibuka FM
26 January 2026, 2:13 pm

Mji wetu wa Maswa ni mkubwa unahitajika usafi wa mara kwa mara, unapoitoa treka site hasa kipindi hiki cha mvua tunaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa yanayotokana na uchafu wa mazingira- “Caroline shayo Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo Maswa”
Wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo Maswa wamelalamika kukithiri kwa uchafu katika mji huo kutokana na trekta linalotumika katika shughuli za kuzoa taka kubadilishiwa matumizi hali inayoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.
Wakichangia katika kikao cha baraza la mamlaka cha robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2025/2026 wajumbe hao wamesema kuwa trekta linalotumika kuzoa taka limekuwa likifanya shughuli za kilimo na kusomba matofali na kuacha shughuli za kukusanya taka hali inafanya taka kurundikana na kuufanya mji wa Maswa kuwa mchafu.

Caroline Shayo ni Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo Maswa akamtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kutoa ufafanuzi wa kina kwanini trekta imebadilishiwa matumizi yake yaliyokusudiwa ya kukusanya na kuzoa taka na badala yake linafanya kazi za kilimo na shughuli za ujenzi na kuacha uchafu ukikithiri katika Mamlaka ya mji huo.
Akitolea ufafanuzi kuhusu trekta la kuzoa taka kubadilishiwa matumizi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri , Vivian Christian amesema kuwa trekta wamesharikabidhi kwa Mtendaji wa mamlaka, hivyo wanapolihitaji wawasiliane ili kujua lipo sehemu gani na linafanya kazi ipi na kwa muda gani

Aidha akitoa taarifa utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo Maswa Bi Veronica Mbiha, ndugu Keneth Julius amesema kuwa ukusanyaji wa mapato umeongezeka ambapo katika kipindi cha robo ya kwanza mamlaka imekusanya zaidi ya shilingi Milioni 76.6 sawa na asilimia 76.6 % ya makisio ya makusanyo yote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi – ccm Wilaya ya Maswa ndugu Onesmo Makota amewapongeza mamlaka kwa jitihada za ukusanyaji wa mapato hivyo kuwataka waongeze bidii zaidi ili kufikia malengo na hatimae kupanda kuwa Halmashauri ya Mji.

