Sibuka FM
Sibuka FM
21 November 2025, 8:51 pm

Wataalamu wa kilimo sitaki kuwaona maofisini nataka niwakute mashambani mkiwasaidia wakulima kuzalisha kwa tija ili kuondokana na malalamiko ya kushuka kwa bei ya pamba angalau mkulima azalishe kilo elfu moja kwa ekari Moja ” DC Vicent Naano Anney ”
Msimu wa Kilimo cha zao la Pamba 2025/2026 umezinduliwa rasmi wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya wakulima kuanza zoezi la upandaji wa mbegu za Pamba kwa mjibu wa kalenda ya Bodi ya pamba Tanzania pamoja kilimo cha mazao mengine.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe, Dkt Vicent Naano Anney na kutoa maagizo kwa maafisa kilimo ngazi ya Wilaya na kata kuhakikisha wanatoka maofisini na kwenda kuwahudumia wakulima ili kuongeza tija ya uzalishaji
Aidha Mhe Anney amesema kuwa mara nyingi wakulima wamekuwa wakipata hasara katika zao za Pamba kwakuzalisha kilo chache za pamba hivyo kuwataka walime kitaalamu na kufuata kanuni bora za kilimo cha zao hilo huku akitoa mifano ya maeneo mengine yaliyoweza kuzalisha zaidi ya kilo elfu moja kwa ekari moja

Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Kaimu mkuu wa division ya Kilimo Halmashauri ya wilaya Maswa ndugu Gimu Yohana Mbabula ametaja malengo ya kilimo kwa msimu wa mwaka huu pamoja na mikakati ya Halmashauri katika kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la pamba

Baadhi ya wakulima waliohudhuria uzinduzi huo wamezungumza na SIBUKA FM na kuelezea matarajio yako katika msimu huu baada ya kupewa elimu na maelekezo kuhusu namna ya uzalishaji wenye tija katika zao la Pamba
Naye diwani mteule wa kata ya Mwamashimba kupitia chama cha mapinduzi – ccm ambapo zoezi la uzinduzi wa msimu wa kilimo cha Pamba kwa mwaka 2025/2026 ndugu Saida Daudi Dila ameishukuru Serikali kwa kutoa zana za kilimo na pembejeo za ruzuku kwa wakulima ili kuleta hamasa ya kulima zao la pamba

