Sibuka FM
Sibuka FM
21 October 2025, 8:39 pm

“Jamii inahitaji sasa elimu ya hali ya juu ya kulinda tamaa za kimwili maana pamoja na kuwa na sheria kali zilizotungwa lakini bado tu jamii inafanya vitendo vya ukatili kwa watoto.”
Na,Daniel Manyanga
Mahakama ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu imemhukumu ,Saimon Nzumbi Magumba mkazi wa kijiji cha Lali miaka 30 jela kwa kosa la kubaka mtoto wake wa kambo wa miaka 10 katika kesi ya jinai shauri Na.20929/2025 iliyosemwa tarehe 20.10.2025.
Mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Itilima,Mhe.Robert Petro Kaanwa, mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa polisi ,Jaston Mhule amesema mshitakiwa ,Saimon Nzumbi Magumba mwenye miaka 38 mkazi wa kijiji cha Lali alishitakiwa katika mahakama ya wilaya ya Itilima kwa kosa moja la kubaka ambapo ni kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2023 .
Mwendesha mashtaka huyo ameiambia Mahakama hiyo kuwa mnamo tarehe 24/08/2025 katika Kijiji cha Lali ndani ya wilaya ya Itilima mzazi wa mhanga alibaini mtoto wake mwenye umri wa miaka 10 amebakwa na baba yake mlezi baada ya yeye kurudi kutoka safari ,
taarifa zilifika kituo cha polisi ambapo mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Itilima kwa mahojiano baada ya upelelezi kukamilika ilibainika kuwa mshtakiwa alikua akimbaka mhanga nyakati za usiku kwa siku ambazo mke wake alikua amesafiri .
Mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa polisi, Jaston Mhule amesema kuwa mshtakiwa alifikishwa mahakamani mnamo tarehe 27/08/2025 kwa ajili ya kesi kuanza ambapo upande wa mashtaka walileta mashahidi 04 na kielelezo 01 vilitolewa mahakamani hapo ili kuthibitisha kesi hiyo.
Kwa upande wa mshtakiwa alipewa nafasi ya kijitetea ambapo aliiomba mahakama hiyo imupunguzie adhabu kwa kuwa yeye ni kosa la kwanza huku upande wa mashtaka ukiiomba mahakama utoe adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa jamii nzima yenye lengo la kubaka kwani matukio kama hayo yanamadhara makubwa kwa mhanga kisaikolojia.
Akitoa hukumu hiyo baada ya kujiridhisha bila kuacha shaka yoyote kutoka pande zote mbili za jamhuri na mshtakiwa kuwa ,Saimon Nzumbi Magumba alitenda kosa hilo huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai ndipo hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Itilima, Mhe.Robert Petro Kaanwa akamhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kubaka mtoto wake wa kambo mwenye miaka 10.