Sibuka FM

Luth wa Mwanundi jela miaka 30 kwa kumbaka mwanaye

10 September 2025, 8:31 am

Muonekano wa nje wa jengo la mahakama ya wilaya ya Maswa ilipo fanyika hukumu ya ,Luth Jacob kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na kosa la kubaka mwanafunzi Picha na Daniel Manyanga

“Kuna kila sababu sasa kwa mamlaka za kutunga sheria kukubali kuwa sheria walizotunga siyo kali na wala wananchi waovu hawaziogopi tena hizo adhabu maana kila kukicha matukio ya ukatili wa kinjisia yanatokea sasa ipo haja ya kurudi tena darasani tuje na sheria kali ambazo zitakuwa na suluhu kwa makosa kama haya”.

Na, Daniel Manyanga

Mahakama  ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu,Luth Jacob (50) Msukuma mkulima mkazi wa kijiji cha Mwanundi kata ya Sengwa wilayani Maswa mkoani Simiyu kwenda jela miaka 30  na kulipa fidia kwa muhanga kiasi cha shilingi laki tatu kwa kosa la kubaka  mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Mwanundi mwenye umri wa miaka 15 mtoto wa mdogo wake na mke wa mshtakiwa. 

Kwenye picha ni wakili mwandamizi wa serikali kutoka ofisi ya mashtaka ya Taifa wilaya ya Maswa,Violeth Mushumbusi akiwa Kwenye moja ya shughuli za Kimahakama Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm

Mbele ya hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa, Mhe. Enos Missana , Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi ,Vedastus Wajanga amesema kuwa mshtakiwa ,Luth Jacob mkazi wa kijiji cha Mwanundi kata ya Sengw’a  alitenda kosa hilo mnamo tarehe ambazo hazikufahamika za mwezi October mwaka 2023 majira ya usiku huko katika kijiji cha Mwanundi wilayani Maswa.

Awali mahakamani hapo ilidaiwa na upande wa Jamhuri ambao uliwakilishwa na wakili wa serikali mwandamizi, Violeth Mushumbusi na mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilaya ya Maswa, mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga, kuwa mshtakiwa alimbaka na kisha kumpa ujauzito (Mimba) mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Mwanundi mwenye umri wa miaka 15 ambae jina lake limehifadhiwa kwa  mujibu wa sheria ili kulinda usalama wa mtoto huyo.

Mwendesha mashtaka huyo ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa katika tarehe ambazo hazikufahamika ya mwezi October. 2023 majira ya usiku mshtakiwa akiwa nyumbani kwake alimwacha mkewe kitandani akiwa amelala usinginzi mzito Kisha akaingia chumba alichokuwa amelala muhanga na watoto wenzake kisha kumbaka na kumpa ujauzito muhanga huyo ambaye ni mtoto wa mdogo wake na mkewe.

Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka  wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga amesema kuwa kosa la  Kubaka ni kinyume na  kifungu cha130 (1)(2)(e) na 131 (1) cha  sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .

Wajanga amesema kuwa mshtakiwa alikamatwa na mtendaji wa kijiji hicho kwa kushiriana na mtendaji wa kata hiyo ,kamanda wa Sungusungu wa kijiji na walimu wa shule ya msingi Mwanundi baadae kufikishwa katika kituo cha polisi wilaya ya Maswa kwa ajili ya mahojiano zaidi ambapo mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na baada ya upelelezi kukamilika mshtakiwa alipandishwa kizimbani huku upande wa mashtaka ulileta mashahidi Sita  na kielelezo kimoja ambacho  PF3.

Mara baada ya utetezi huo Kukamilika mahakama hiyo ilimtia hatia mshtakiwa, Luth Jacob huku mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kumpatia adhabu kali mshtakiwa huyo ili iwe funzo kwake na jamii kwani makosa ya kubaka, kumpa ujauzito (Mimba) yanaongezeka katika jamii na yanaleta athari kubwa kwa muhanga kisakolojia,kijamii,kiuchumi , kiafya pia makosa kama haya ni ukatili wa kijinsia katika jamii na hatimaye  kusababisha maradhi au kifo kwa muhanga pamoja na kuacha makovu yasiyofutika maishani.

Akitoa hukumu hiyo ya jinai kesi Na.12270/2025  iliyotolewa  mnamo tarehe 09.09.2025  na hakimu mkazi  mfawidhi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa, Mhe.Enos Missana mara baada ya kusikiliza utetezi wa pande zote mbili za mshtakiwa na Jamhuri bila kuacha mashaka yoyote ndipo mahakama ikamhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kulipa fidia kwa muhanga kiasi cha shilingi laki tatu kosa la Kubaka ,Kumpa ujauzito (Mimba) mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Mwanundi  wilayani Maswa mwenye umri wa miaka 15 huku adhabu zote hizo zinatumika kwa pamoja kwa maana ya Concurrently.