Sibuka FM
Sibuka FM
18 August 2025, 10:23 am
“Kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji siyo utajiri bali ni kuwakumbuka wenye uhitaji kama vitabu vitakatifu vya dini vinavyosema kuwa dini ya kweli ni kuwakumbuka wenye uhitaji hivyo basi jamii yenye uwezo ni bora ikawa na moyo wa kuwakumbuka wenzetu wenye uhitaji “.
Na,Anitha Balingilaki
Umoja wa watuma salamu nchini UWASATA umefanya mkutano mkuu ambao umeenda sambamba na uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa ngazi ya kitaifa watakaoongoza umoja huo 2025/28 kwa mujibu wa katiba ya umoja huo.
Baadhi ya viongozi waliochaguliwa wametetea nyadhifa zao akiwemo mwenyekiti taifa Abubakari Sendeu kutokea Dar es salaam ambaye alikuwa akitetea nafasi yake na makamu mwenyekiti taifa Lenga Chapati alitokea Simiyu naye alikuwa akitetea nafasi yake.
Wengine waliochaguliwa ni katibu mkuu wa umoja huo ,Fadhili Bakari anatokea Magugu ambaye alikuwa akitetea nafasi yake, mhasibu ni Abisalim Msuya anatokea Dar es salaam, Msemaji wa umoja huo ,Musa Mjengi anatokea Dar es salaam ambaye alikuwa akitetea nafasi yake,msemaji msaidizi ,Pius Kipeta anatokea Mpanda, mkuu wa nidhamu, Mlumba Mlumba anatokea Nzega mkoani Tabora.
Wengine waliochaguliwa ni wajumbe wa umoja huo akiwemo ,Hadija Omari kutoka Morogoro,Yusuph Khamis anatokea Shinyanga, Kassim Bakari anatokea Manyara na Laider Sima anatokea Singida.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huu umoja huo ulifika hospitali ya halmashauri ya mji wa Bariadi na kutoa msaada kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo na miongoni mwa vitu vilivyotolewa ni pamoja na sabuni na mafuta ya kupaka.
Makamu mwenyekiti wa umoja huo, Lenga Chapati amesema kuwa umoja huo utaendelea kuikumbuka jamii yenye uhitaji kila mara wanapokutana na kuiunganisha pamoja ili nao wasiweze kuona kama jamii imewatenga.
Nao baadhi ya watuma salamu walioshiriki mkutano huo wameiomba jamii iwe na moyo wa kujitoa kwa ajili ya watu wengine wenye uhitaji ili kuleta faraja kwa jamii hiyo.


