Sibuka FM
Sibuka FM
19 June 2025, 4:54 pm

“Elimu ni urithi pekee ambao mtu hawezi kuporwa na mtu yeyote hivyo tuwekeze elimu kwa watoto wetu bila kujali kuna ajira au hakuna ajira maana huu ni ujuzi wake ambao utakuja kumsaidia katika maisha ya hapa duniani”.
Na, Daniel Manyanga
Imeelezwa kuwa utekelezaji wa mradi wa shule bora unaolenga kuinua ubora, ushirikishwaji na mazingira salama ya kujifunzia kwa wasichana na wavulana wote katika shule za msingi za serikali umetajwa kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi katika halmashauri ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Hayo yamesemwa na mratibu wa mradi huo katika halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Felister Mwanga wakati akizungumza na walimu wakuu, maafisa elimu kata na walimu wa taaluma wa halmashauri hiyo kwa ajili ya kufanya tathimin ya mradi wa shule bora unaofadhiliwa na (UKaid) ambapo ameeleza namna ulivyosaidia kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na shule ambazo huko nyuma zilikuwa hazifanyi vizuri kitaaluma lakini kupitia mradi huo zimeongeza ufaulu wa wanafunzi.
Kwa upande wake afisa elimu wa kata ya Gambosi na mwezeshaji wa kitaifa wa masuala ya KKK na SRP ,Edward Kashindye amewasisitiza walimu wa madarasa ya awali, la kwanza na la pili kuzingatia matumizi ya zana na kona za ujifunzaji kwa wanafunzi wao ili kuwasaidia kuelewa kwa urahisi wanachofundishwa darasani.
Elice Samuel, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ibulyu na Protas Shayo ,mwalimu mkuu shule ya msingi Igaganulwa ni baadhi ya walimu walioshiriki katika tathimin hiyo wameeleza umuhimu wa matumizi ya zana na kona za ujifunzaji katika ufundishaji kwa wanafunzi wa madarasa ya chini.
