Sibuka FM
Sibuka FM
12 June 2025, 5:42 pm

“Rushwa ni adui wa haki na maendeleo kahuna rushwa kubwa wala ndogo nendeni tukawahudumia wananchi walio na changamoto za kunyanyaswa na watu wanaotumia madaraka kwa kuwakandamiza watu ambao walitakiwa wapewe haki hakuna aliye mkubwa zaidi ya sheria na katiba ya nchi”.
Na, Daniel Manyanga
Katika kuhakikisha vitendo vya rushwa vinapungua na hata kumaliza kabisa hapa nchini Waziri wa nchi, ofisi ya Rais, menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora,George Simbachawene, ameitaka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) kuweka jitihada kubwa katika mapambano ya rushwa za aina zote bila kujali kubwa au ndogo ili kuwaondolea kero wananchi zinazosababishwa na vitendo vya rushwa.

Simbachawene ametoa maagizo hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la TAKUKURU mkoa wa Simiyu na kusisitiza kuwa ni muhimu taasisi hiyo ikavishughulikia vitendo vyote vya rushwa ambavyo vinasababisha wananchi kushindwa kupata haki zao kutokana na wachache kutokuwa waaminifu au kutumia vyeo vyao,ukubwa wao na umaarufu wao kukandamiza haki za wengine.
Awali akitoa taarifa juu ya ujenzi wa jengo hilo, mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU ,Crispin Chalamila ametaja gharama zilizotumika katika ujenzi huo, huku mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Simiyu, Manyama Tungaraza akieleza litakavyosaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi hiyo mkoani Simiyu.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu ,Kenani Kihongosi, ameeleza kulidhishwa na utendaji wa TAKUKURU mkoani Simiyu, huku mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsha Mohammed, akiomba kesi za TAKUKURU kuendeshwa kwa uharaka ili kuwasaidia wananchi kupata haki zao hivyo kuondoa mianya ya rushwa kwa wale wanataka kununua haki.

