Sibuka FM
Sibuka FM
24 May 2025, 8:25 pm

“Sekta ya miundombinu ya barabara ni Moja kati ya ajenda muhimu Sana kwa ustawi wa jamii yetu maana ndiyo inayotumika kusafirishia mazao mbalimbali kutoka huko kijijini kuja sehemu za masoko lakini ikitaka kufungua uchumi wako lazima Kwanza ufungue barabara zako ziweze Kupitia kwa urahisi na muda wote”.
Na, Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Dkt.Vicent Anney amewataka wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) wilayani hapo kutafuta namna nyingine ya kutengeneza barabara ya kijiji cha Mwamashindike kata ya Mwabalatulu ili iweze kupitika kwa urahisi kwa wananchi wakati wakiwa wanasubiri bajeti kubwa kutokana na uharibifu mkubwa wa barabara hiyo.


Mkuu huyo wa wilaya ,Dkt.Anney ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho wa kusikiliza kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi ambapo wananchi wakaibua hoja ya barabara hiyo kuwa mbovu kwa muda mrefu hivyo kushindwa kuitumia katika shughuli za uzalishaji.
Awali Renard Masanja, Yunus Bukundi na Sanga Salum wakiwa katika mkutano huo wa hadhara wamesema kwasasa wanatumia muda mrefu kufika maeneo mengine kutokana na ubovu wa barabara hali ambayo inawalazimu kuzunguka kupitia vijiji vya Budekwa na Kiloleli hivyo kushindwa kuzifikia huduma za kijamii kwa wakati pale wanapokuwa wanahitaji huduma hizo

Akijibia changamoto hiyo ya barabara kaimu meneja TARURA wilayani hapo, Edward Jinayi amesema kuwa barabara hiyo ina mito mingi hali iliyopelekea kuomba kibali maalum kutokana na gharama zake za matengenezo kuwa kubwa hali iliyopelekea kuchelewa kwa ukarabati huo.