Sibuka FM
Sibuka FM
8 May 2025, 1:35 pm

Niwaombe maafisa Usafirishaji muwe na tabia ya kujiwekea akiba kutokana na kipato chenu mnachopata kwani hii Kazi ya bodaboda huwezi kuifanya katika Maisha yako yote itafika wakati umri utagoma kuendesha pikipiki ” Dc Dkt Vicent Anney “
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu Dkt Vicent Naano Anney amewataka maafisa Usafirishaji maarufu kwa jina la Bodaboda kuhakikisha wanatii Sheria za Usalama barabarani pamoja na kutoa Ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kubaini wahalifu huku akiwaomba waunde vikundi ili kupata Bodaboda za Mkopo unaotolewa na Halmashauri kutokana na ukusanyaji wa Mapato ya ndani
Amesema hayo baada ya kukutana na Kundi la Vijana hao waliojiajiri kupitia shughuli za bodaboda na kusikiliza Changamoto wanazokutana nazo katika biashara hiyo ili Serikali ione namna ya kuweza kuwasaidia
Aidha Dkt Anney amewataka waendesha bodaboda hao kuwa na tabia ya kuwekeza katika aseti mbalimbali kutokana na kipato cha shughuli wanazofanya kwani kazi hiyo hawawezi kuifanya katika Maisha yao yote kutokana na umri unavyoenda.

Mkuu wa Usalama barabarani Wilayani hapa, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi James Nyorobi amewataka waendesha boda boda kuzingatia sheria za barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu, kubeba mishikaki na kuzingatia matumizi ya taa za kuongozea magari

Nao baadhi ya bodaboda walioshiriki kikao hicho cha Mkuu wa Wilaya wakapata nafasi ya kupaza sauti zao kuhusu Elimu ya sheria za barabarani pamoja na matukio ya uhalifu na Wizi wa Pikipiki yanayoendelea wilayani hapa