Sibuka FM

Jumanne jela miaka 30,fidia laki tano kwa kubaka mwanafunzi wa sekondari Maswa

30 April 2025, 2:34 pm

Muonekano wa nje wa jengo la mahakama ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ambapo mshtakiwa , Jumanne Clement amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kulipa fidia ya shilingi laki tano kwa muhanga Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm

Kuna kila sababu sasa kwa mamlaka za kutunga sheria kukubali kuwa sheria walizotunga siyo kali na wala wananchi waovu hawaziogopi tena hizo adhabu maana kila kukicha matukio ya ukatili wa kinjisia yanatokea sasa ipo haja ya kurudi tena darasani tuje na sheria kali ambazo zitakuwa na suluhu kwa makosa kama haya”.

Na, Daniel Manyanga

Mahakama  ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu Jumanne Clement (23) Msukuma mkulima mkazi wa kijiji cha Ngudu wilayani Kwimba mkoani Mwanza kwenda jela miaka 30  na kulipa fidia kwa muhanga kiasi cha shilingi laki tano kwa  makosa matatu ya Kubaka,Kumpa ujauzito (Mimba) na Kupoka mwanafunzi wa shule ya sekondari Jijabilishi mwenye umri wa miaka 15.

Kwenye picha ni wakili wa serikali mwandamizi kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo,Violeth Mushumbusi akiwa kwenye moja ya majukumu ambapo naye kwenye kesi hii alisimama kwa upande wa Jamhuri Picha kutoka Sibuka Fm

Mbele ya hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa, Mhe. Enos Missana , Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi ,Vedastus Wajanga amesema kuwa mshtakiwa ,Jumanne Clement mkazi wa kijiji cha Ngudu wilayani Kwimba alitenda kosa hilo mnamo tarehe 20 April 2024 majira ya usiku huko katika kijiji cha Jijabilishi wilayani Maswa.

Awali mahakamani hapo ilidaiwa na upande wa Jamhuri ambao uliwakilishwa na wakili wa serikali mwandamizi, Violeth Mushumbusi na mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilaya ya Maswa, mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga, kuwa mshtakiwa alimbaka na kisha kumpa ujauzito (Mimba) mwanafunzi wa shule ya sekondari Jijabilishi mwenye umri wa miaka 15 ambae jina lake limehifadhiwa kwa  mujibu wa sheria ili kulinda usalama wa mtoto huyo na badae alimchukua muhanga kwenda kuishi naye kama mme na mke wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka  wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga amesema kuwa kosa la kwanza  Kubaka ni kinyume na  kifungu cha130 (1)(2)(e) na 131 (1) cha  sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .

Kosa la pili Kumpa ujauzito (Mimba) mwanafunzi ni kinyume na kifungu cha 60A(3) cha sheria ya elimu sura ya 353 iliyofanyiwa marejeo ya mwaka 2002 na kama ilivyofanyiwa mabadiliko madogo katika kifungu cha 22 cha sheria ya mabadiliko ya madogo namba 2 ya mwaka 2016 huku kosa la tatu Kupoka (Abduction) ni kinyume na kifungu cha 134 na 34 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Wajanga amesema kuwa taarifa zilifika kituo cha polisi  Ngudu wilayani Kwimba ambapo mshtakiwa alikamatwa na baadae kusafirishwa nakufikishwa katika kituo cha polisi wilaya ya Maswa na mshtakiwa alipohojiwa alikiri kitendo makosa hayo na baada ya upelekezi kukamilika mshtakiwa alifikishwa Mahakamani ambapo upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano na vielelezo vinne ikiwemo PF3 ya muhanga na maelezo ya onyo kwa mshtakiwa huku  mshtakiwa naye alipewa nafasi ya kuwasilisha utetezi wake ambapo alikili kufanya kitendo hicho na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na anategemewa na familia.

Mara baada ya utetezi huo Kukamilika mahakama hiyo ilimtia hatia mshtakiwa, Jumanne Clement huku mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kumpatia adhabu kali mshtakiwa huyo ili iwe funzo kwake na jamii kwani makosa ya kubaka, kumpa ujauzito (Mimba) yanaongezeka katika jamii na yanaleta athari kubwa kwa muhanga kisakolojia,kijamii,kiuchumi , kiafya pia makosa kama haya ni ukatili wa kijinsia katika jamii na hatimaye  kusababisha maradhi au kifo kwa muhanga pamoja na kuacha makovu yasiyofutika maishani.

Akitoa hukumu hiyo ya jinai kesi Na.23752/2024 iliyotolewa  leo hii mnamo tarehe 29.April.2025  na hakimu mkazi  mfawidhi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa, Mhe.Enos Missana mara baada ya kusikiliza utetezi wa pande zote mbili za mshtakiwa na Jamhuri bila kuacha mashaka yoyote ndipo mahakama ikamhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kulipa fidia kwa muhanga kiasi cha shilingi laki tano kwa makosa matatu ya Kubaka ,Kumpa ujauzito (Mimba) na Kupoka (Abduction) mwanafunzi wa shule ya sekondari Jijabilishi wilayani Maswa mwenye umri wa miaka 15 huku adhabu zote hizo zinatumika kwa pamoja kwa maana ya Concurrently.