Sibuka FM
Sibuka FM
15 April 2025, 8:42 pm

“Matukio ya ubakaji yamekuwa yakiongezeka kila siku, je, jamii yetu haina uelewa wa madhara kwa mhanga au sheria zetu hazina ukali wa kumaliza kesi hizi kama ni hivyo basi kuna kila sababu sasa kwa mamlaka husika kukaa chini na kuziangalia upya sheria zetu ili kumlinda muhanga“.
Na Daniel Manyanga
Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu Kassimu Masagyo Mwiburi (50) mkulima mkazi wa kijiji cha Njiapanda ya Malampaka kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka mwanafunzi wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 11.
Mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Maswa, Mhe. Aziz Khamis, Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi ,Vedastus Wajanga amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 26 Februari 2025 majira ya usiku huko katika kijiji cha Njiapanda wilayani hapo.
Awali mahakamani hapo ilidaiwa na upande wa Jamhuri ambao uliwakilishwa na wakili wa serikali mwandamizi Suzan Masule na Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilaya ya Maswa, mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga, kuwa mshtakiwa alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 11 mwanafunzi wa shule ya msingi ambapo jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya kulinda usalama wa mtoto huyo.
Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo mkaguzi msaidizi wa polisi, Vedastus Wajanga amesema kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha130 (1)(2)(e) na 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022 .
Wajanga amesema kuwa taarifa zilifika kituo cha polisi wilaya ya Maswa ambapo mshtakiwa alikamatwa na alipohojiwa katika kituo hicho alikataa kabisa kufanya kitendo hicho na baada ya upelelezi kukamilika mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa hatua zingine za kisheria ambapo upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano na vielelezo viwili ili kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo na baada ya ushahidi huo kutolewa mshtakiwa naye alipewa nafasi ya kuwasilisha utetezi wake ambapo alikili kufanya kitendo hicho na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na anategemewa na familia.
Mara baada ya utetezi huo Kukamilika mahakama hiyo ilimtia hatia mshtakiwa, Kassimu Masagyo Mwiburi huku mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kumpatia adhabu kali mshtakiwa huyo ili iwe funzo kwake na jamii kwani makosa ya kubaka yanaongezeka katika jamii na yanaleta athari kubwa kwa muhanga kisakolojia,kijamii,kiuchumi , kiafya pia makosa kama haya ni ukatili wa kijinsia katika jamii na hatimaye kusababisha maradhi au kifo kwa muhanga pamoja na kuacha makovu yasiyofutika maishani.
Akitoa hukumu hiyo ya jinai kesi Na.6282/2025 iliyotolewa leo hii mnamo tarehe 15.April.2025 na hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Mhe.Azizi Khamis mara baada ya kusikiliza utetezi wa pande zote mbili za mshtakiwa na Jamhuri bila kuacha mashaka yoyote ndipo mahakama ikamhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka mwanafunzi wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 11.