

2 April 2025, 8:04 pm
“Hivi hatuwezi kumaliza kabisa suala la fisi mkoani hapa? Siku chache zilizopita matukio kama haya yaliripotiwa katika wilaya za Itilima na Maswa leo hii wameingia mjini Bariadi je, ni kweli hatuwezi au ndiyo kusema bado hatujaamua kufanya hivyo? Naomba kwenye hili sungusungu wapewe nafasi kumaliza shida hii ni fikra zangu tu lakini”.
Na, Daniel Manyanga
Kondoo wapatao 21 wameuawa na kundi la fisi lililovamia kwenye zizi nyumbani kwa Mageni Maduhu wilayani Bariadi mkoani Simiyu majira ya saa nne usiku wa April mosi mwaka huu.
Akizungumza na Sibuka FM mapema leo ilipofika kwa ajili ya kushuhudia tukio ,Mageni Maduhu amesema mnamo majira ya saa tano usiku alisikia sauti za fisi wakilia ndipo alitoka nje kuangalia nini kinaendelea alikuta kondoo 21 wameuliwa kati ya hao wapo kondoo wa kuposea binti kwa ajili ya kijana wake kupata mke.
Mangu Mangolyo ni mwenyekiti wa Mtaa huo amesema kuwa tukio hilo ni la kushangaza kwani halijawahi kusikika au kuona fisi wanashambulia au kula kondoo wengi kiasi hicho mara zote fisi huchukua kondoo mmoja na kwenda naye tofauti na kilichotokea.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamekiri kuwepo kwa wanyama hao mjini Bariadi huku wakitilia shaka usalama wa mifugo yao na kuomba serikali ione namna ya kumaliza shida hiyo ya fisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga amefika katika familia hiyo iliyokumbwa na tukio na kutoa pole huku akitangaza msako mkali wa wanyama hao kutokana na kupokea taarifa za uwepo wa wanyama hao mjini humo.