Maswa: Mtoto wa miaka 4 afariki kwa kushambuliwa na fisi
24 January 2025, 7:40 pm
“Matukio ya fisi kuvamia na kushambulia wananchi hadi kupoteza maisha hatuwezi kuyaacha tu yaendelee lazima tuone namna nzuri ya kushughulikia ili kuondoa maswali mengi kwa wananchi kujiona kama wao wametengwa katika usalama na ulinzi “.
Na, Daniel Manyanga
Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Aswege Kaminyoge ameagiza askari wa wanyamapori kwa kushirikiana na jeshi la jadi sungusungu kufanya msako usiku na mchana wa mnyama fisi kufuatia tukio la kushambuliwa kwa mtoto Khija Ntubanga miaka 4 hadi kufariki katika kijiji cha Ilambambasa kata ya Senani wilayani hapo.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani hapo ametoa agizo hilo baada ya kufika kijijini hapo na kujionea namna tukio lilivyotokea na kuacha majonzi katika familia hiyo kufuatia mtoto wao kufariki dunia kwa kushambuliwa na fisi kutokana na kujeruhiwa sehemu ya viungo vya mwili wake na mnyama huyo.
Aswege Kaminyoge amesema kuwa tukio hilo limetokea Januari 22 mwaka huu majira ya saa 1:00 jioni katika kitongoji cha Ilambambasa ambapo wananchi walimwona fisi huyo akimshambulia mtoto mita 15 kutoka nyumbani kwao ndipo walipopiga kelele ya kuomba msaada na fisi alimwachia mtoto na kukimbilia katika shamba lililo karibu na nyumba hiyo.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ilambambasa wamesema kuwa msako wa kumtafuta fisi huyo ulianza mara moja kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori kwani bila kufanya hivyo watashindwa kufanya kazi zao za kilimo kwa kuhofia kushambuliwa na fisi hasa kwa watoto wanaobaki nyumbani.