Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kutumia Bil 47.2 Mwaka wa Fedha 2025/2026
20 January 2025, 10:57 am
Bajeti hii imezingatia Miongozo na Sera mbalimbali pamoja na Vipaumbele Muhimu kwa wananchi wa Maswa “DED Maswa Ndugu Maisha Mtipa”
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoa Simiyu limepitisha Bajeti ya Shilingi Bilioni 47. 2 kwa ajili ya Matumizi kwa mwaka wa Fedha ujao 2025/2026 ikiwa ni Ongezeko la asilimia 0.81 % ya Bajeti ya mwaka 2024/2025 ambayo ilikuwa Bilioni 46.8
Akiwasilisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Ndugu Julius Ikongora amesema kuwa Bajeti hiyo imekuwa na Ongezeko kutokana na kuongezeka kwa Mapato ya ndani ya Halmashauri
Amesema kuwa katika Makadirio hayo ya Mpango wa Bajeti yamezingatia Miongozo na Sera mbalimbali kama vile Dira ya Taifa, Malengo 17 ya maendeleo endelevu ya mwaka 2015-2035 pamoja na maelekezo ya Viongozi wa Kitaifa, Chama Tawala na Wizara.
Baada ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Bajeti hiyo baadhi ya Madiwani katika Halmashauri hiyo Stephen Dwese, Esther Ng’holongo na Bundala Isambaja wakapata nafasi ya Kuchangia na kuwapongeza waandaaji kwani imelenga mambo muhimu ya Wananchi wa Wilaya ya Maswa.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoulizwa na Madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndugu Maisha Mtipa amesema halmashauri imejipanga kuboresha maeneo hasa eneo la Nh’ami kunakojengwa Viwanda na Jengo la Utawala la Halmashauri hiyo.
Baada ya majadiliano ya Rasimu ya Bajeti hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe Paul Maige akawahoji Madiwani na kuipitisha kuwa Bajeti rasmi ya mwaka wa Fedha 2025/2026.