Maswa:Witness, Dwese mahakamani kwa kumshambulia diwani wa Zanzui
11 January 2025, 11:50 am
“Baraza la madiwani ni sehemu moja muhimu sana kwa wananchi kujuwa diwani wao anapeleka shida zao na kutafutiwa ufumbuzi sasa wananchi wanasubiri maendeleo leo wanasikia diwani kapigana na diwani sidhani kama ndiyo agenda ya Taifa.”
Na, Daniel Manyanga
Diwani wa viti maalumu na diwani wa kata ya Ng’wigwa (Mme na Mke) wa chama cha mapinduzi CCM wilayani Maswa mkoani Simiyu wamefikishwa mahakamani kwa kumshambulia kwa lugha chafu ya matusi na kumsababishia majeraha ya mwili diwani mwenzao wa kata ya Zanzui , Jeremia Mange Shigala maarufu kwa jina la Makondeko wakati wa kikao cha baraza la madiwani kikiendelea wilayani hapo.
Kesi hiyo ya jinai namba 36038/2024 imetaja leo hii tarehe 10.01.2025 katika mahakama ya wilaya ya Maswa mbele ya hakimu mkazi mwandamizi,Mhe.Enoss Missana ikiwahusiwa diwani wa viti maalumu wa chama cha mapinduzi CCM, Witness Philipo Dwese na diwani wa kata ya Ng’wigwa, Stephen Dwese ambao ni (Mke na Mme) kwa kosa la kumtolea lugha chafu ya matusi na kumshambulia na kumsababishia majeraha ya mwili diwani wa kata ya Zanzui wa chama cha mapinduzi CCM, Jeremia Mange Shigala maarufu kwa jina la Makondeko.
Mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Maswa Mhe.Enoss Missana mwendesha mashtaka mwandamizi kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo,Vailet Mshumbusi amesema kuwa mnamo tarehe 23.08.2024 mshitakiwa namba moja , Witness Philipo Dwese anashitakiwa kwa kosa la kumshambulia kwa lugha chafu ya matusi na kosa la pili ni kumshambulia na kumsababishia majeraha ya mwili wakiwa na diwani mwenzake , Stephen Dwese(Mke na Mme) diwani wa kata ya Zanzui, Jeremia Mange Shigala maarufu kwa jina la Makondeko wakati wa kikao cha baraza la madiwani kikiendelea.
Mwendesha mashtaka mwandamizi kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani Maswa, Vailet Mshumbusi amesema kuwa kosa la Kwanza la kumshambulia kwa lugha chafu ya matusi diwani wa kata ya Zanzui ni kinyume cha kifungu namba 89(1)(a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Kosa la pili ni kumshambulia na kumsababishia majeraha ya mwili diwani wa kata ya Zanzui, Jeremia Mange Shigala maarufu kwa jina la Makondeko ambapo ni kinyume cha kifungu namba 241 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 ambapo tukio hilo walilitenda mshitakiwa namba moja na mshitakiwa namba mbili ,Witnes Philipo Dwese na Stephen Dwese kwa pamoja walimpa kichapo diwani mwenzao hali iliyopelekea kushindwa kuendelea na kikao hicho kutokana na maumivu makali aliyoyapata baada ya kushushiwa kipigo hicho.
Washtakiwa wote kwa pamoja wamekana mashtaka hayo huku mwendesha mashtaka mwandamizi kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka wilayani hapo, Vailet Mshumbusi akisema kuwa upelelezi umekamilika tayari kwa kesi kuendelea ambapo hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Maswa,Mhe.Enoss Missana ameipangia tarehe 23.01.2025 tayari kwa kuanza kusikilizwa kutokana na upelelezi kukamilika.