Binadamu waathiri pori la akiba Kijereshi
7 January 2025, 8:34 pm
“Shughuli za kibinadamu ni changamoto nyingine katika kuhifadhi mapori ya akiba tunakila sababu jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kulinda tuzu zetu”.
Na, Daniel Manyanga
Wananchi waishio pembezoni mwa pori la akiba Kijereshi lililopo katika wilaya za Bariadi na Busega mkoani Simiyu, wametakiwa kuacha uvamizi na kufanya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo malisho ya(Kuchungia) mifugo, kukata miti, kulima na uwindaji haramu katika eneo la hifadhi ya pori hilo kwani kufanya hivyo ni kuenenda kinyume cha sheria za uhifadhi hapa nchini.
Rai hiyo imetolewa na afisa mhifadhi mwandamizi wa pori la akiba la Kijereshi kutoka mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) ,Rogathe Wado wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa maeneo yanayozunguka pori hilo, walipotembelea eneo hilo kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani na kuzitaja shughuli mbalimbali zinazofanywa katika pori hilo ambazo zipo kinyume cha sheria,kanuni na taratibu za mamlaka ya uhifadhi hapa nchini.
Akizungumza na Sibuka fm redio mkuu wa kituo cha polisi Lamadi,Mrakibu wa polisi,Emmanuel Shani amewataka wananchi waishio pembezoni mwa maeneo ya hifadhi kutoa taarifa za vitendo vya uvamizi hifadhini ili kupambana na watu hao wasiokuwa na nia njema katika kutunza hifadhi hiyo.
Magreth Izengo, Edward Ochogo na Haji Malongo ni baadhi ya viongozi wa maeneo yanayozunguka pori la akiba la Kijereshi wakaeleza namna watakavyoshirikiana na mamlaka za uhifadhi katika kukabiliana na tatizo la uvamizi wa pori hilo.