Wafugaji Itilima watakiwa kutoingiza mifugo hifadhini
6 January 2025, 8:43 pm
“Mifugo inachangia pato la Taifa lakini hatuwezi kuacha maeneo ya hifadhi hapa nchini yaharibiwe na wafugaji wasiotaka kufuata sheria,kanuni na taratibu za uhifadhi katika kulinda uoto wa asili ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.”
Na, Daniel Manyanga
Wafugaji waishio pembezoni mwa maeneo ya hifadhi nchini wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwemo kutoingiza mifugo yao katika maeneo hayo kwa ajili ya malisho ili kuepuka kuingia kwenye migogoro na mamlaka za uhifadhi hali ambayo inapelekea baadhi ya wafugaji kutaifishwa kwa mifugo hao.
Rai hiyo imetolewa na mlezi wa chama cha wafugaji Tanzania (CCWT),Joseph Makongolo alipokutana na kuzungumza na wafugaji wa kata za Nkuyu,Ndolelezi,Chinamili,Mwaswale na Mhunze zilizopo wilayani Itilima mkoani Simiyu na kuwataka wafugaji kufuata Sheria zilizowekwa na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kulinda hifadhi ili kuepuka kuwa sehemu ya migogoro na mamlaka za uhifadhi hapa nchini.
Samson Joseph,Ngwelu Kayanda,Yenga Bulengela na Malingo Kelebe ni baadhi ya wafugaji walioshiriki kikao hicho ambapo wametaja changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuiomba serikali izitafutie ufumbuzi wake.