TCB yagawa baiskeli 218 kwa wakulima wezeshi wa pamba Maswa
16 December 2024, 8:51 pm
“Mkoa wa Simiyu ni mmoja wapo wa mkoa unaozalisha Pamba nyingi hapa nchini hivyo kuwa zao mkuu la kibiashara na lakimkakati zaidi.”
Na, Daniel Manyanga
Katika kuhakikisha kilimo cha zao la Pamba kinawatoa wakulima kimaisha bodi ya Pamba Tanzania (TCB) wilayani Maswa mkoani Simiyu imegawa baiskeli 218 kwa wakulima wawezeshaji ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora na chenye tija.
Akikabidhi baiskeli hizo kwa wakulima wawezeshaji mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa lengo la baiskeli hizo ni kurahisisha utendaji kazi na kuongeza uzalishaji wa Pamba ,kulima kwa tija ili kuongeza thamani ya zao hilo hasa kwa wakulima.
Ally Mabruki ni mkaguzi wa bodi ya pamba wilaya ya Maswa amesema kuwa kukabidhi baiskeli hizo kwa wakulima wawezeshaji ni kuongeza uzalishaji na kulima kwa tija ili wakulima waweze kujikwamua na umasikini wa kipato.
Veronica Paul na Malita Sasa, ni baadhi ya wakulima wawezeshaji waliopata vitendea kazi hivyo wamesema kuwa watahakikisha wanafanya kazi iliyokusudia hasa kuleta thamani ya zao la Pamba kwa wakulima.
Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amewataka wakulima wawezeshaji kuzitumia baiskeli hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na bodi ya Pamba wilayani hapo na siyo vinginevyo.