Ripoti ya mkaguzi wa hesabu za ndani kuamua malipo ya wenyeviti Maswa
19 September 2024, 5:25 pm
“Katika kuhakikisha madeni yote yanalipwa kwa wadai wote halmashauri ya wilaya ya Maswa imesubiria ripoti ya mkaguzi wa hesabu za ndani ili wenyeviti wapate haki zao”.
Na, Daniel Manyanga
Wajumbe wa mamlaka ya mji mdogo wa Maswa mkoani Simiyu ambao ni wenyeviti wa vitongoji wa kata nne katika mji wa Maswa ambazo ni Sola, Nyalikungu ,Binza na Shanwa wametoa wito kwa serikali kuhakikisha wanalipwa malimbikizo ya madai ya fedha zao zinazokadiliwa kufikia milioni 152 wanazodai kabla ya kumaliza muda wao wa kiutawala Oktoba 25 mwaka huu ili kupisha uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika November 27 mwaka huu.
Wenyeviti hao wametoa ombi hilo kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika katika ukumbi wa mamlaka ya mji mdogo Maswa na kuhudhuriwa na wajumbe wa baraza hilo ambapo moja ya agenda ikaibuliwa ni lini fedha zao zitalipwa maana zimekuwa za muda mrefu wanadai bila ya kuwa na mafanikio yoyote.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo Maswa,Agustino Kabuta amesema kuwa malimbikizo ya madai ya wenyeviti yanatokana na posho za madalaka na vikao yanaharibu heshima ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kutokana na watu wachache kushindwa kumsaidia katika utendaji kazi wao kutokana na yeye kuwa na kazi nyingi za kufanya hivyo ameomba kufanya mapitio upya ya madai ya wajumbe hao ili waweze kupata haki yao kabla ya kumaliza kwa muda wa kiutawala.
Awali Mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Henry Kagimbo Rweyemamu ambaye ni afisa utumishi wa halmashauri hiyo amesema kuwa wanasubiri ripoti ya mkaguzi wa hesabu za ndani hivyo amewaomba wenyeviti hao kuwa na subira.