Sibuka FM

Maswa: Serikali yaombwa kuwekeza kwenye elimu jumuishi kwa watoto,vijana

17 June 2024, 1:21 pm

Pichani ni mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Maswa girls,Mwl Kuyunga Jackson aliyekaa katikati ya wachungaji wa makanisa yanayotoa huduma ya mtoto na vijana Picha na Daniel Manyanga

Elimu jumuishi kwa watoto na vijana itasaidia sana kupunguza wimbi la watoto mitaani na utegemezi wa ajira kutoka serikalini hivyo tusiogope kuwekeza kwenye elimu jumuishi.”

Na Daniel Manyanga

Wadau wa maendeleo kwa watoto na vijana wilayani Maswa mkoani Simiyu wameomba serikali kuwekeza kwenye elimu jumuishi kwa watoto hali ambayo itapunguza utegemezi wa ajira kutoka serikalini kwa wahitimu wa fani mbalimbali.

Ombi hilo limetolewa na waratibu wa huduma ya mtoto na vijana kutoka shirika la Compassion,Flavian Ignatius kutoka kituo cha T.A.G Ebenezer Maswa na Reuben Joshua kutoka huduma ya mtoto na vijana kituo cha P.A.G.T Unyanyembe  wakati wa maadhimisho ya mtoto wa Afrika kwa makanisa yanayotoa huduma ya mtoto wilayani hapo.

Sauti za waratibu wa huduma ya mtoto na vijana kutoka Compassion klasta ya Maswa

Awali mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Maswa girls,Mwl Kuyunga Jackson amewaomba wazazi na walezi kuwapatia muda watoto wao ili waweze kujifunza ujuzi mbalimbali katika vituo vya huduma ya mtoto na vijana hali ambayo itapunguza wimbi la watoto wa mtaani pamoja na kuwa waangalifu katika matumizi ya mitandao ya kijamii.

Sauti ya mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Maswa girls

Kwa upande wake ,Suzan Francis ni mmoja wa wazazi waliohudhuria maadhimisho hayo amesema kuwa kupitia shirika la Compassion limewasaidia katika malezi na makuzi ya watoto kwa kumpatia nafasi ya kujifunza stadi za kazi hali ambayo itawasaidia watoto wao kuwa na ujuzi pindi wanapokuwa na umri mkubwa waweze kujiajiri na siyo kusubiri ajira serikalini hivyo wazazi wawape nafasi ya kujifunza.

Sauti ya mmoja wa wazazi wakielezea manufaa yanayoyapata kutoka Shirika la Compassion

Wakisoma risala kwa mgeni rasmi, Letisia Kulwa na Salome Raphael wamesema kuwa pamoja na mafanikio wanayoyapata katika vituo vya huduma ya mtoto na vijana lakini bado kuna changamoto mbalimbali zinazowabili katika vituo ikiwemo muda wa masomo ya shuleni kuingiliana pamoja na upungufu wa walimu wa kufundisha ujuzi kuwa wachache.

Sauti ya watoto wakisoma risala na kuelezea changamoto katika vituo.

Maadhimisho ya mtoto wa Afrika hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 16 June ili kuwakumbuka watoto waliouwawa katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini wakati wakidai haki zao huku kaulimbiu ya mwaka huu “Elimu jumuishi izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi”