DC Simalenga awapa za uso wakulima makanjanja wa pamba
7 June 2024, 11:15 am
“Msimu ujao wa kilimo hatutaruhusu mkulima yeyote kuchukua mbegu na viatilifu bila kuonesha shamba lake alilolima ili kuondoa wakulima makanjanja katika zao hilo”
Na, Daniel Manyanga
Serikali wilayani Bariadi mkoani Simiyu imebaini uwepo wa ekari elfu arobaini hewa za zao la pamba kutokana na uwepo wa watu wasiokuwa wakulima kuchukua viatilifu, mbegu na kwenda kufanya biashara katika maduka yao ya kilimo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kusikiliza kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi ambapo amesema changamoto za zao la pamba zinasababishwa na watu wachache wasiokuwa waaminifu wanaochukua mbegu na madawa wakati siyo wakulima wa zao hilo na kupeleka katika biashara zao.
Simalenga amesema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/24 zaidi ya ekari elfu arobaini zilibainika kuwa hewa kutokana na watu wasiokuwa wakulima kuchukua madawa na mbegu hivyo msimu wa kilimo ujao hakuna mkulima atakayepewa madawa au mbegu bila kuonesha shamba lake alipolima ili kuondoa udanganyifu katika zao hilo ambalo ni utambulisho wa mkoa wa Simiyu.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi baadhi ya wakulima Marco Samson na Seni Naraja wameomba serikali kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto katika zao hilo la pamba ili mkulima aweze kupata tija kutokana na kile alichokifanya kwa msimu mzima hali ambayo itaweza kuwavutia hata watu wengine kuingia kwenye kilimo cha zao hilo.
Kwa upande wake katibu wa chama cha wanunuzi wa pamba nchini Boaz Ogolla amesema kuwa bei ya pamba kutokuwa rafiki kwa mkulima ni kutokana na uhitaji wa soko la kimataifa na mwenendo wake ukoje na kuna vigezo ambavyo vinaangaliwa kama bei ya mbegu inauzwaje hivyo wakulima walime kwa kufuata kilimo bora hali itakayoweza kuondokana na changamoto ya bei hata kama ikiwa chini.