Zaidi ya kaya 413 hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko Busega
7 May 2024, 7:33 pm
Faida ya kufuatilia taarifa za mamlaka ya hali ya hewa kumetajwa kusaidia kujikinga na kuepuka madhara yatokanayo na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Na Daniel Manyanga
Kaya zaidi 413 kutoka vitongoji vitatu vya Itongo, Lamadi na Makanisani katika kata ya Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu zipo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na makazi yao kuzingirwa na maji ya ziwa Victoria kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hatua iliyopelekea baadhi ya kaya kulazimika kuyahama makazi huku wengine wakiendelea kubaki japokuwa nyumba zao zipo kwenye maji.
Wakizungumza na Sibuka Fm ilipofika kujionea madhara hayo wakazi wa maeneo hayo wanasema kuwa siyo mara ya kwanza maji ya ziwa Victoria kuyafuata makazi yao huku wengine wakiiomba serikali kuwapatia mahema badala ya kuwapeleka kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya wahanga wa tukio pamoja na kuona namna nzuri ya kuweka mazingira rafiki yatakayoweza kuwaepusha na magonjwa ya mlipuko.
Bija Laurent ni diwani wa kata ya Lamadi na Athuman Said ni balozi wa nyumba kumi wameiomba serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kufanyiwa kwa marekebisho ya mto Lamadi ili uweze kupitisha maji yake bila ya kuwaathiri wakazi kwani mto huo umekuwa chanzo cha kuzingirwa kwa nyumba hizo.
Akizungumza na Sibuka Fm kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Busega ,Faiza Salim amesema kuwa tayari serikali ya wilaya hiyo kupitia kamata ya maafa imeanza kuchukua hatua ili kukabiliana na changamoto hiyo hasa kwa wananchi ambao nyumba zao zipo hatarini.
Faiza Salim ametoa wito kwa wananchi kuondoka mara moja katika makazi yao yaliyozingirwa na maji Ili kujiepusha na madhara makubwa ambayo yanaweza kujitokeza.