Mpango wa chakula mashuleni kuongeza ufaulu wa wanafunzi Bariadi
18 April 2024, 4:40 pm
Chakula mashuleni ni swala la muhimu sana katika kukuza maendeleo ya wanafunzi kwenye ufaulu wa mitihani yao kitaifa na hivyo itapunguza utoro kwa wanafunzi mashuleni.
Na,Daniel Manyanga
Wazazi na Walezi wa wanafunzi katika shule ya msingi Imalilo iliyopo halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu wamechangia magunia 39 ya mahindi ,magunia matatu ya maharage na kiasi cha shilingi laki sita na elfu sabini na nane ili kuwezesha wanafunzi kupata uji na chakula cha mchana hatua itakayoweza kuongeza ufaulu katika mitihani ya kitaifa na kupunguza utoro.
Wakizungumza na Sibuka fm wakati wanakabidhi mahitaji hayo kwa shule hiyo Wazazi na Walezi hao wamesema kuwa wameamua kuchanga kutokana na shule hiyo kuonesha njia ya kuwapatia uji na chakula cha mchana ambapo kupitia mashamba ya shule hiyo imeweza kuvuna kiasi cha magunia 31ya mahindi ambayo yote yataenda kutumika kwenye mpango wa chakula shuleni hapo.
Wakipokea mahitaji hayo Geofrey Kamugisha ni mwalimu mkuu wa shule hiyo na Peter Luhumbila mwenyekiti wa kamati ya shule wamewaomba wazazi na walezi ambao bado hawajachangia kushiriki zoezi hilo muhimu ili kuwezesha wanafunzi 1601 kupata uji na chakula cha mchana hali ambayo utaweza kupunguza utoro na kuongeza ufaulu shuleni hapo.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Bariadi,Adrian Jungu amesema shule hiyo ni mfano wa kuigwa kwenye halmashauri hiyo huku mkuu wa wilaya ya Bariadi,Simon Simalenga akitoa maagizo kwa shule zote wilayani hapo.