LAAC yaipongeza Maswa kwa usimamizi mzuri wa miradi
28 March 2024, 10:19 am
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa – LAAC imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa Usimamizi Mzuri wa Fedha za Miradi ya Maendeleo zinazoletwa Wilayani hapo.
Akitoa Pongezi hizo mara baada ya kutembelea Jengo la Wagonjwa wa Dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe, Suma Fyandomo amesema kuwa Jengo hilo ni la kisasa kabisa ukilinganisha na Majengo mengine ya Dharura waliyotembelea katika maeneo mbalimbali.
Akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Ujenzi wa Mradi wa Jengo la Wagonjwa wa Dharura Mganga Mfawidhi wa wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa Dr James Bwire amesema kuwa Jengo hilo limekuwa Msaada mkubwa katika Utoaji wa Huduma za Dharura kwa wagonjwa
Kwa Upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC Mhe, Stanslaus Mabula amesema kuwa Mradi wa Kiwanda cha Chaki ni wakipekee sana kwa Ukanda huu hivyo shauku ya Serikali na Watanzania nikuona Mradi huu unaleta Manufaa huku akitoa mwezi Mmoja ili uanze kufanya kazi.
Baadhi ya Wananchi Wilayani hapa wameishukuru Serikali kwa kujenga Jengo hilo ambalo limesogeza huduma kwani hapo awali walikuwa wakipa shida kupeleka Wagonjwa Hospitali ya kanda ya Bugando na Kutumia Gharama kubwa .
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe, Paul Maige amemshukuru Rais Samia kwakuleta Fedha nyingi kwa ajili ya Utekelezaji wa Miradi hiyo ya Kimkakati huku akiahidi kutekeleza Ushauri wote uliotolewa na Kamati hiyo ya LAAC mara baada ya kutembelea Jengo la Wagonjwa wa Dharura katika Hospitali ya Maswa na Ujenzi wa Kiwanda cha Chaki.